Waebrania 10:1-18
1
Sheria ni kivuli tu cha mambo mema yajayo, wala si uhalisi wa mambo yenyewe. Kwa sababu hii, haiwezekani kamwe kwa njia ya dhabihu zitolewazo mwaka hadi mwaka kuwakamilisha wale wanaokaribia ili kuabudu.
2
Kama dhabihu hizo zingeweza kuwakamilisha, hazingeendelea kutolewa tena. Kwa kuwa hao waabuduo wangekuwa wametakaswa mara moja tu, wala wasingejiona tena kuwa na dhambi.
3
Lakini zile dhabihu zilikuwa ukumbusho wa dhambi kila mwaka,
4
kwa sababu haiwezekani damu ya mafahali na mbuzi kuondoa dhambi.
5
Kwa hiyo, Kristo alipokuja duniani, alisema: “Dhabihu na sadaka hukuzitaka, bali mwili uliniandalia;
6
sadaka za kuteketezwa na za dhambi hukupendezwa nazo.
7
Ndipo niliposema, ‘Mimi hapa, nimekuja, imeandikwa kunihusu katika kitabu: Nimekuja kuyafanya mapenzi yako, Ee Mungu.’ ”
8
Kwanza alisema, “Dhabihu na sadaka, sadaka za kuteketezwa na za dhambi hukuzitaka, wala hukupendezwa nazo” (ingawa sheria iliagiza zitolewe).
9
Kisha akasema “Mimi hapa, nimekuja kuyafanya mapenzi yako.” Aondoa lile Agano la kwanza ili kuimarisha la pili.
10
Katika mapenzi hayo sisi tumetakaswa na kufanywa watakatifu kwa njia ya sadaka ya mwili wa Yesu Kristo alioutoa mara moja tu.
11
Kila kuhani husimama siku kwa siku akifanya huduma yake ya ibada, na kutoa tena na tena dhabihu zile zile ambazo haziwezi kamwe kuondoa dhambi.
12
Lakini huyu kuhani akiisha kutoa dhabihu moja kwa ajili ya dhambi kwa wakati wote, aliketi mkono wa kuume wa Mungu.
13
Tangu wakati huo anangoja mpaka adui zake wawekwe chini ya miguu yake,
14
kwa sababu kwa dhabihu moja amewafanya kuwa wakamilifu milele wale wote wanaotakaswa.
15
Pia Roho Mtakatifu anatushuhudia kuhusu jambo hili. Kwanza anasema:
16
“Hili ndilo Agano nitakalofanya nao baada ya siku hizo, asema Bwana. Nitaziweka sheria zangu mioyoni mwao, na kuziandika katika nia zao.”
17
Kisha aongeza kusema: “Dhambi zao na kutokutii kwao sitakumbuka tena.”
18
Basi haya yakiisha kusamehewa, hakuna tena dhabihu yoyote inayotolewa kwa ajili ya dhambi.
Settings