Mwanzo 41:39-46
39
Ndipo Farao akamwambia Yosefu, “Maadamu Mungu amekufunulia yote haya, hakuna mwingine yeyote mwenye akili na hekima kama wewe.
40
Wewe utakuwa msimamizi wa jumba langu la kifalme, na watu wangu wote watatii amri zako. Ni kuhusu kiti cha ufalme tu nitakuwa mkuu kuliko wewe.”
41
Kwa hiyo Farao akamwambia Yosefu, “Sasa nakuweka uwe msimamizi wa nchi yote ya Misri.”
42
Ndipo Farao akaivua pete yake ya muhuri kutoka kidoleni mwake na kuivalisha katika kidole cha Yosefu. Akamvika majoho mazuri ya kitani safi na mkufu wa dhahabu shingoni mwake.
43
Akampandisha katika gari lake la farasi kama msaidizi wake, watu wakatangulia wakishangilia, wakisema, “Fungueni njia!” Ndivyo Farao alivyomweka Yosefu kuwa msimamizi wa nchi yote ya Misri.
44
Kisha Farao akamwambia Yosefu, “Mimi ni Farao, lakini pasipo neno lako, hakuna mtu mwenye ruhusa kuinua mkono au mguu katika nchi yote ya Misri.”
45
Farao akamwita Yosefu Safenath-Panea, pia akampa Asenathi binti Potifera, kuhani wa mji wa Oni, kuwa mke wake. Ndipo Yosefu akaitembelea nchi yote ya Misri.
46
Yosefu alikuwa na miaka thelathini alipoingia katika utumishi wa Farao mfalme wa Misri. Naye Yosefu akatoka mbele ya Farao akasafiri katika nchi yote ya Misri.
Settings