Skip to content
Ezra 9:6-15

Ezra 9:6-15

6
Nami nikaomba: “Ee Mungu wangu, natahayari na kuona aibu kukuinulia uso wangu Mungu wangu, kwa sababu dhambi zetu zimejikusanya hata kupita juu ya vichwa vyetu na hatia yetu imefika mbinguni.
7
Tokea siku za babu zetu mpaka sasa, hatia yetu imekuwa kubwa. Kwa sababu ya dhambi zetu, sisi na wafalme wetu na makuhani wetu tumekabiliwa na vita, utumwa, kutekwa na kudhiliwa katika mikono ya wafalme wa kigeni, kama ilivyo leo.
8
“Lakini sasa, kwa muda mfupi, Bwana Mungu wetu amekuwa na neema kwa kutuachia mabaki na kutupa mahali imara katika mahali pake patakatifu, hivyo Mungu wetu atupa mwanga machoni petu na unafuu katika utumwa wetu.
9
Ingawa tu watumwa, Mungu wetu hajatuacha katika kufungwa kwetu. Ametuonyesha huruma mbele ya wafalme wa Uajemi: Ametujalia maisha mapya kwa kujenga upya nyumba ya Mungu wetu na kukarabati magofu yake, naye ametupa ukuta wa ulinzi katika Yuda na Yerusalemu.
10
“Lakini sasa, Ee Mungu wetu, tunaweza kusema nini baada ya hili? Kwa maana tumedharau maagizo
11
uliyoyatoa kupitia watumishi wako manabii uliposema: ‘Nchi mnayoiingia kuimiliki ni nchi iliyochafuliwa na uovu wa watu wake. Kwa matendo yao ya machukizo wameijaza nchi kwa unajisi wao kutoka mwisho mmoja hadi mwingine.
12
Kwa hiyo, msiwaoze binti zenu kwa wana wao wala binti zao kwa wana wenu. Msitafute mkataba wa urafiki nao kwa wakati wowote. Ndipo mtakapofanikiwa na kula mema ya nchi na kuwaachia watoto wenu nchi hiyo kama urithi wao wa milele.’
13
“Yale yaliyotupata ni matokeo ya matendo yetu mabaya, pia hatia yetu kubwa. Hata hivyo, wewe Mungu wetu, umetuadhibu kidogo kuliko dhambi zetu zilivyostahili na umetupa mabaki kama haya.
14
Je, tutavunja maagizo yako tena na kuoana na watu ambao hufanya mambo ya machukizo? Je, hutakuwa na hasira ya kutosha juu yetu na kutuangamiza, bila kutuachia mabaki wala atakayenusurika?
15
Ee Bwana, Mungu wa Israeli, wewe ni mwenye haki! Leo hii tumeachwa kama mabaki. Tupo hapa mbele zako na hatia yetu, ingawa katika hali hii hakuna hata mmoja wetu anayeweza kusimama mbele zako.”
Settings

Reading Style

Typeface

Font Size 19px

Options