Ezra 9:10-15
10
“Lakini sasa, Ee Mungu wetu, tunaweza kusema nini baada ya hili? Kwa maana tumedharau maagizo
11
uliyoyatoa kupitia watumishi wako manabii uliposema: ‘Nchi mnayoiingia kuimiliki ni nchi iliyochafuliwa na uovu wa watu wake. Kwa matendo yao ya machukizo wameijaza nchi kwa unajisi wao kutoka mwisho mmoja hadi mwingine.
12
Kwa hiyo, msiwaoze binti zenu kwa wana wao wala binti zao kwa wana wenu. Msitafute mkataba wa urafiki nao kwa wakati wowote. Ndipo mtakapofanikiwa na kula mema ya nchi na kuwaachia watoto wenu nchi hiyo kama urithi wao wa milele.’
13
“Yale yaliyotupata ni matokeo ya matendo yetu mabaya, pia hatia yetu kubwa. Hata hivyo, wewe Mungu wetu, umetuadhibu kidogo kuliko dhambi zetu zilivyostahili na umetupa mabaki kama haya.
14
Je, tutavunja maagizo yako tena na kuoana na watu ambao hufanya mambo ya machukizo? Je, hutakuwa na hasira ya kutosha juu yetu na kutuangamiza, bila kutuachia mabaki wala atakayenusurika?
15
Ee Bwana, Mungu wa Israeli, wewe ni mwenye haki! Leo hii tumeachwa kama mabaki. Tupo hapa mbele zako na hatia yetu, ingawa katika hali hii hakuna hata mmoja wetu anayeweza kusimama mbele zako.”
Settings