Ezekieli 26:1-14
1
Mwaka wa kumi na moja, siku ya kwanza ya mwezi, neno la Bwana likanijia kusema:
2
“Mwanadamu, kwa sababu Tiro amesema kuhusu Yerusalemu, ‘Aha! Lango la kwenda kwa mataifa limevunjika, nayo milango yake iko wazi mbele yangu, sasa kwa kuwa amekuwa magofu nitastawi.’
3
Kwa hiyo hili ndilo Bwana Mwenyezi asemalo: Mimi niko kinyume na wewe, ee Tiro, nami nitaleta mataifa mengi dhidi yako, kama bahari inayovurumisha mawimbi yake.
4
Watavunja kuta za Tiro na kuibomoa minara yake, nitakwangua udongo wake na kuufanya mwamba mtupu.
5
Itakuwa huko katikati ya bahari patakuwa mahali pa kutandaza nyavu za kuvulia samaki, kwa maana nimenena, asema Bwana Mwenyezi. Atakuwa nyara kwa mataifa,
6
nayo makao yake huko bara yataangamizwa kwa upanga. Ndipo watakapojua kwamba Mimi ndimi Bwana.
7
“Kwa maana hili ndilo Bwana Mwenyezi asemalo: Kutoka kaskazini nitamleta dhidi ya Tiro Mfalme Nebukadneza wa Babeli, mfalme wa wafalme, akiwa na farasi na magari ya vita, wapanda farasi na jeshi kubwa.
8
Atayaharibu makao yako huko bara kwa upanga, ataweka jeshi kukuzingira, atakuzingira mpaka kwenye kuta za ngome zako na kuinua ngao zake dhidi yako.
9
Ataelekeza mapigo ya vyombo vyake vya kubomolea dhidi ya kuta zako na kubomoa minara yako kwa silaha zake.
10
Farasi zake zitakuwa nyingi sana kiasi kwamba utafunikwa na mavumbi watakayotimua. Kuta zako zitatikisika kwa mshindo wa farasi wa vita, magari makubwa na magari ya vita wakati aingiapo malango yako kama watu waingiao mji ambao kuta zake zimebomolewa kote.
11
“Kwato za farasi zake zitakanyaga barabara zako zote, atawaua watu wako kwa upanga na nguzo zako zilizo imara zitaanguka chini.
12
Watateka utajiri wako na kuchukua nyara bidhaa zako, watazivunja kuta zako na kuzibomoa nyumba zako nzuri, watatupa baharini mawe yako, mbao zako na kifusi chako.
13
Nitakomesha kelele za nyimbo zako, na uimbaji wako wa kinubi kamwe hautasikika tena.
14
Nitakufanya mwamba mtupu, nawe utakuwa mahali pa kutandazia nyavu za kuvulia samaki. Kamwe hutajengwa tena, kwa maana Mimi Bwana nimenena, asema Bwana Mwenyezi.
Settings