Kutoka 32:26-34
26
Kwa hiyo Mose akasimama kwenye ingilio la kambi, akasema, “Yeyote aliye upande wa Bwana, aje upande wangu.” Walawi wote wakamjia.
27
Ndipo alipowaambia, “Hili ndilo Bwana, Mungu wa Israeli asemalo: ‘Kila mmoja wenu ajifunge upanga wake kiunoni aende huku na huko kambi yote mwisho hadi mwisho mwingine, kila mmoja amuue ndugu yake, na rafiki yake na jirani yake.’ ”
28
Walawi wakafanya kama Mose alivyoamuru, siku ile wakafa watu wapatao 3,000.
29
Kisha Mose akasema, “Leo mmewekwa wakfu kwa Bwana, kwa kuwa mlikuwa kinyume na wana wenu wenyewe na ndugu zenu, naye Mungu amewabariki leo.”
30
Siku iliyofuata Mose akawaambia watu, “Mmefanya dhambi kubwa. Lakini sasa nitapanda juu kwa Bwana, labda nitaweza kufanya upatanisho kwa ajili ya dhambi yenu.”
31
Hivyo Mose akarudi kwa Bwana na kumwambia, “Lo! Hawa watu wamefanya dhambi kubwa namna gani! Wamejitengenezea miungu ya dhahabu.
32
Lakini sasa nakusihi, wasamehe dhambi yao; lakini kama sivyo, basi nifute kutoka kwenye kitabu ulichoandika.”
33
Bwana akamjibu Mose, “Yeyote aliyenitenda dhambi ndiye nitakayemfuta kutoka kwenye kitabu changu.
34
Sasa nenda, uongoze hao watu mpaka mahali nilipokuambia, naye malaika wangu atakutangulia. Pamoja na hayo, wakati utakapofika wa mimi kuwaadhibu, nitawaadhibu kwa ajili ya dhambi yao.”
Maandiko ya Biblia: Biblica® Open Kiswahili Contemporary Version (Neno: Bibilia Takatifu)™, © 1984, 1989, 2009, 2015 Biblica, Inc. · CC BY-SA 4.0“Biblica” is a trademark registered in the United States Patent and Trademark Office by Biblica, Inc., used with permission.
Settings