Waefeso 5:3-14
3
Lakini uasherati, usitajwe miongoni mwenu, wala uchafu wa aina yoyote, wala tamaa, kwa sababu mambo haya hayastahili miongoni mwa watakatifu.
4
Wala pasiwepo mazungumzo machafu ya aibu, au maneno ya upuzi au mzaha, ambayo hayafai, badala yake mshukuruni Mungu.
5
Kwa habari ya mambo haya mjue hakika kwamba: Msherati, wala mtu mwovu, wala mwenye tamaa mbaya, mtu kama huyo ni mwabudu sanamu, kamwe hataurithi Ufalme wa Kristo na wa Mungu.
6
Mtu yeyote na asiwadanganye kwa maneno matupu, kwa kuwa hasira ya Mungu huwaka kwa sababu ya mambo kama haya juu ya wale wasiomtii.
7
Kwa hiyo, msishirikiane nao.
8
Kwa maana zamani ninyi mlikuwa giza, lakini sasa ninyi ni nuru katika Bwana. Enendeni kama watoto wa nuru
9
(kwa kuwa tunda la nuru hupatikana katika wema wote, haki na kweli),
10
nanyi tafuteni yale yanayompendeza Bwana.
11
Msishiriki matendo ya giza yasiyofaa, bali yafichueni.
12
Kwa maana ni aibu hata kutaja mambo yale ambayo wasiotii wanayafanya sirini.
13
Lakini kila kitu kilichowekwa nuruni, huonekana,
14
kwa kuwa nuru ndiyo hufanya kila kitu kionekane. Hii ndiyo sababu imesemekana: “Amka, wewe uliyelala, ufufuke kutoka kwa wafu, naye Kristo atakuangazia.”
Settings