Skip to content
Kumbukumbu 4:1-14

Kumbukumbu 4:1-14

1
Sikia sasa, ee Israeli, amri na sheria nitakazokufundisha wewe. Zifuate ili upate kuishi na uingie kuimiliki nchi ambayo Bwana, Mungu wa baba zako anawapa.
2
Usiongeze wala usipunguze chochote ninachowaamuru ninyi, ila myashike maagizo ya Bwana Mungu wenu ambayo nawapa.
3
Mliona kwa macho yenu wenyewe kile Bwana alichokifanya kule Baal-Peori. Bwana Mungu wenu aliwaangamiza kutoka miongoni mwenu kila mmoja aliyemfuata Baali wa Peori,
4
lakini ninyi nyote mlioshikamana na Bwana kwa uthabiti, Mungu wenu, mko hai mpaka leo.
5
Tazama, nimewafundisha amri na sheria kama Bwana Mungu wangu alivyoniamuru mimi, ili mzifuate katika nchi mnayoiingia kuimiliki.
6
Zishikeni kwa uangalifu, kwa kuwa hii itaonyesha hekima na ufahamu wenu kwa mataifa, ambayo yatasikia kuhusu amri zote hizi, nao watasema, “Hakika taifa hili kubwa ni watu wenye hekima na ufahamu.”
7
Ni taifa gani jingine lililo kubwa kiasi cha kuwa na miungu yao iliyo karibu nao kama Bwana Mungu wetu alivyo karibu nasi wakati wowote tunapomwomba?
8
Nalo ni taifa gani jingine lililo kubwa hivi lenye kuwa na amri na sheria za haki kama hizi ninazoweka mbele yenu leo?
9
Mwe waangalifu, na makini ili msije mkasahau mambo ambayo mliyaona kwa macho yenu, wala kuyaacha yaondoke moyoni mwenu siku zote za uhai wenu. Mwafundishe hayo watoto wenu na watoto wao baada yao.
10
Kumbuka siku uliyosimama mbele za Bwana Mungu wako kule Horebu, wakati aliponiambia, “Wakutanishe watu mbele yangu wasikie maneno yangu ili kwamba waweze kujifunza kuniheshimu kwa muda wote watakaoishi katika nchi, nao waweze kuwafundisha watoto wao maneno hayo.”
11
Mlisogea karibu na mkasimama chini ya mlima wakati ulipowaka moto mpaka mbinguni juu, pamoja na mawingu meusi na giza nene.
12
Ndipo Bwana alipozungumza nanyi kutoka moto. Mkasikia sauti ya maneno lakini hamkuona umbo, kulikuwa na sauti tu.
13
Aliwatangazia Agano lake na Amri Kumi, ambazo aliwaamuru mzifuate, kisha akaziandika juu ya vibao viwili vya mawe.
14
Naye Bwana alinielekeza wakati huo kuwafundisha ninyi sheria na amri ambazo mnapaswa kuzifuata katika nchi ambayo mnavuka Yordani kuimiliki.
Settings

Reading Style

Typeface

Font Size 19px

Options