Matendo 28:17-29
17
Siku tatu baadaye Paulo akawaita pamoja viongozi wa Kiyahudi. Walipokwisha kukusanyika akawaambia, “Ndugu zangu, ingawa sikufanya jambo lolote dhidi ya watu wetu au dhidi ya desturi za baba zetu, lakini nilikamatwa huko Yerusalemu nikakabidhiwa kwa Warumi.
18
Wao walipokwisha kunihoji, wakataka kuniachia huru kwa sababu hawakuona kosa lolote nililolifanya linalostahili adhabu ya kifo.
19
Lakini Wayahudi walipopinga uamuzi huo, nililazimika kukata rufaa kwa Kaisari, ingawa sikuwa na lalamiko lolote juu ya taifa langu.
20
Basi hii ndiyo sababu nimewatumania, ili niseme nanyi. Kwa kuwa ni kwa ajili ya tumaini la Israeli nimefungwa kwa minyororo.”
21
Wakamjibu, “Hatujapokea barua zozote kutoka Uyahudi zinazokuhusu, wala hapana ndugu yeyote aliyekuja hapa ambaye ametoa taarifa au kuzungumza jambo lolote baya juu yako.
22
Lakini tungependa kusikia kutoka kwako unalofikiri kwa sababu tunajua kwamba kila mahali watu wanazungumza mabaya kuhusu jamii hii.”
23
Baada ya kupanga siku ya kuonana naye, watu wengi wakaja kuanzia asubuhi hadi jioni akawaeleza na kutangaza kuhusu Ufalme wa Mungu akijaribu kuwahadithia juu ya Yesu kutoka Sheria ya Mose na kutoka Manabii.
24
Baadhi wakasadiki yale aliyosema, lakini wengine hawakuamini.
25
Hivyo hawakukubaliana, nao walipokuwa wanaondoka, Paulo akatoa kauli moja zaidi: “Roho Mtakatifu alinena kweli na baba zenu aliposema mambo yale yaliyomhusu Bwana Yesu kwa kinywa cha nabii Isaya kwamba:
26
“ ‘Nenda kwa watu hawa na useme, “Hakika mtasikiliza lakini hamtaelewa; na pia mtatazama, lakini hamtaona.”
27
Kwa kuwa mioyo ya watu hawa imekuwa migumu; hawasikii kwa masikio yao, na wamefumba macho yao. Wasije wakaona kwa macho yao, na wakasikiliza kwa masikio yao, wakaelewa kwa mioyo yao, na kugeuka nami nikawaponya.’
28
“Basi na ijulikane kwenu kwamba, huu wokovu wa Mungu umepelekwa kwa watu wa Mataifa, nao watasikiliza.” [
29
Naye akiisha kusema maneno haya, Wayahudi wakaondoka wakiwa na hoja nyingi miongoni mwao.]
Settings