2 Samweli 11:17-27
17
Wakati watu wa mjini walipotoka kwenda kupigana dhidi ya Yoabu, baadhi ya watu katika jeshi la Daudi wakauawa, zaidi ya hayo, Uria, Mhiti, akafa.
18
Yoabu akampelekea Daudi maelezo yote ya vita.
19
Akamwagiza mjumbe hivi, “Utakapokuwa umemaliza kumpa mfalme maelezo ya vita,
20
hasira ya mfalme yaweza kuwaka, naye aweza kukuuliza, ‘Kwa nini mlisogea karibu hivyo na mji kupigana? Hamkujua kuwa wangeweza kuwapiga mishale kutoka ukutani?
21
Ni nani aliyemuua Abimeleki mwana wa Yerub-Besheth? Je, mwanamke hakutupa juu yake jiwe la juu la kusagia kutoka ukutani, kwa hiyo akafa huko Thebesi? Kwa nini mlisogea hivyo karibu ya ukuta?’ Ikiwa atakuuliza hivi, ndipo umwambie, ‘Pia mtumishi wako Uria, Mhiti, amekufa.’ ”
22
Mjumbe akaondoka. Alipowasili akamwambia Daudi kila kitu alichokuwa ametumwa na Yoabu kusema.
23
Mjumbe akamwambia Daudi, “Watu walituzidi nguvu wakatoka nje ya mji dhidi yetu kwenye eneo la wazi, lakini tuliwarudisha nyuma mpaka kwenye ingilio la mji.
24
Ndipo wapiga upinde walitupa mishale kwa watumishi wako kutoka ukutani, na baadhi ya watu wa mfalme wakafa. Zaidi ya hayo, Uria, Mhiti, mtumishi wako amekufa.”
25
Daudi akamwambia mjumbe, “Ukamwambie Yoabu hivi, ‘Jambo hili lisikutie wasiwasi, upanga hula huyu sawa na ulavyo mwingine. Zidisha mashambulizi dhidi ya mji na uangamize.’ Mwambie Yoabu hivi ili kumtia moyo.”
26
Mke wa Uria aliposikia kwamba mumewe amekufa, akamwombolezea.
27
Baada ya muda wa maombolezo kwisha, Daudi akamtaka aletwe nyumbani kwake, naye akawa mkewe, na akamzalia mwana. Lakini jambo alilokuwa amefanya Daudi lilimchukiza Bwana.
Settings