2 Wafalme 12:8-16
8
Makuhani wakakubali kuwa hawatakusanya tena fedha kutoka kwa watu na kwamba hawatakarabati Hekalu wenyewe.
9
Yehoyada kuhani akachukua kisanduku na akatoboa tundu kwenye kifuniko chake. Akakiweka kando ya madhabahu upande wa kulia unapoingia hekaluni mwa Bwana. Makuhani waliolinda ingilio wakaweka ndani ya kisanduku fedha zote ambazo zililetwa katika Hekalu la Bwana.
10
Kila mara walipoona kuwa kuna kiasi kikubwa cha fedha ndani ya kisanduku, mwandishi wa mfalme na kuhani mkuu walikuja, wakazihesabu fedha hizo zilizoletwa katika Hekalu la Bwana, na kuziweka katika mifuko.
11
Wakiisha kuthibitisha kiasi cha hizo fedha, waliwapa watu walioteuliwa kusimamia kazi katika Hekalu. Kwa fedha hizo, wakawalipa wale watu waliofanya kazi katika Hekalu la Bwana: yaani, maseremala na wajenzi,
12
waashi na wakata mawe. Walinunua mbao na mawe ya kuchongwa kwa ajili ya ukarabati wa Hekalu la Bwana, na kulipia gharama nyingine zote za kulitengeneza.
13
Fedha zilizoletwa kwenye Hekalu hazikutumiwa kutengenezea masinia ya fedha, mikasi ya kusawazishia tambi, mabakuli ya kunyunyizia, tarumbeta wala vyombo vingine vyovyote vya dhahabu au fedha kwa ajili ya Hekalu la Bwana;
14
zililipwa kwa wafanyakazi, ambao walizitumia kwa kukarabati Hekalu.
15
Wao hawakudai kupewa hesabu ya fedha kutoka kwa wale waliowapa ili kuwalipa wafanyakazi, kwa sababu walifanya kwa uaminifu wote.
16
Fedha zilizopatikana kutokana na sadaka za hatia na sadaka za dhambi hazikuletwa katika Hekalu la Bwana; zilikuwa mali ya makuhani.
Settings