1 Samweli 15:1-9
1
Samweli akamwambia Sauli, “Mimi ndiye ambaye Bwana alinituma nikutie mafuta uwe mfalme juu ya watu wake Israeli, basi sasa sikiliza ujumbe kutoka kwa Bwana.
2
Hili ndilo Bwana Mwenye Nguvu Zote asemalo: ‘Nitawaadhibu Waamaleki kwa kile walichowatendea Israeli walipowavizia wakati walipanda kutoka Misri.
3
Basi sasa nenda ukawashambulie Waamaleki na kuwaangamiza kabisa pamoja na kila kitu kilicho mali yao. Usiwahurumie; waue wanaume na wanawake, watoto na wanyonyao, ngʼombe na kondoo, ngamia na punda.’ ”
4
Ndipo Sauli akawaita watu na kuwapanga huko Telaimu, askari wa miguu 200,000 pamoja na watu 10,000 kutoka Yuda.
5
Sauli akaenda katika mji wa Amaleki na kuwavizia bondeni.
6
Kisha akawaambia Wakeni, “Ondokeni, waacheni Waamaleki ili nisije nikawaangamiza ninyi pamoja nao, kwa kuwa ninyi mliwatendea mema Waisraeli wote wakati walipanda kutoka Misri.” Basi Wakeni wakaondoka, wakawaacha Waamaleki.
7
Ndipo Sauli akawashambulia Waamaleki toka Havila mpaka Shuri, hadi mashariki ya Misri.
8
Akamchukua Agagi, mfalme wa Waamaleki akiwa hai, nao watu wake wote akawaangamiza kabisa kwa upanga.
9
Lakini Sauli na hilo jeshi wakamhifadhi hai Agagi na kondoo na ngʼombe walio wazuri, mafahali na wana-kondoo walionona kila kitu kilichokuwa kizuri. Hivi vitu hawakuwa radhi kuviangamiza kabisa, bali kila kitu kilichodharauliwa na kilicho dhaifu wakakiangamiza kabisa.
Settings