1 Samweli 14:6-15
6
Yonathani akamwambia kijana wake mbeba silaha, “Njoo, tuvukie doria ya wale jamaa wasiotahiriwa. Huenda Bwana atatenda kwa ajili yetu. Hakuna chochote kitakachoweza kumzuia Bwana kuokoa, kwamba ni kwa wingi au kwa uchache.”
7
Mbeba silaha wake akamwambia, “Fanya yale yote uliyo nayo katika moyo wako. Songa mbele; moyo wangu na roho yangu viko pamoja nawe.”
8
Yonathani akasema, “Basi njoo; tutavuka kuwaelekea hao watu na kuacha watuone.
9
Kama wakituambia, ‘Subirini hapo mpaka tuje kwenu,’ tutakaa pale tulipo na hatutakwea kwao.
10
Lakini kama watasema, ‘Pandeni mje kwetu,’ tutakwea, kwa sababu hiyo itakuwa ishara yetu kwamba Bwana amewatia mikononi mwetu.”
11
Basi wote wawili wakajionyesha kwa doria ya Wafilisti. Wafilisti wakasema, “Tazama! Waebrania wanatambaa toka mashimoni walimokuwa wamejificha.”
12
Watu wa kwenye doria wakawapigia kelele Yonathani na mbeba silaha wake, wakisema, “Njooni, pandeni kwetu nasi tutawakomesha.” Basi Yonathani akamwambia mbeba silaha wake, “Panda nyuma yangu; Bwana amewatia mikononi mwa Israeli.”
13
Yonathani akapanda juu, akitumia mikono yake na miguu, pamoja na mbeba silaha wake papo hapo nyuma yake. Wafilisti wakaanguka mbele ya Yonathani, naye mbeba silaha wake akamfuata akiwaua nyuma yake.
14
Katika hilo shambulio la kwanza, Yonathani na mbeba silaha wake waliua kama watu ishirini kwenye eneo kama la nusu eka.
15
Kisha fadhaa ikawapata jeshi lote, wale waliokuwa kambini na shambani, wale waliokuwa katika doria na makundi ya washambuliaji, nayo nchi ilitetemeka. Ilikuwa ni hofu ya ghafula iliyotumwa na Mungu.
Settings