Hesabu 8:1-15
1
Bwana akamwambia Mose,
2
“Sema na Aroni umwambie, ‘Wakati utakapoziweka zile taa saba, zinatakiwa kuangaza eneo lililo mbele ya kinara cha taa.’ ”
3
Aroni akafanya hivyo; akaziweka zile taa ili zielekee mbele kwenye kinara cha taa, kama vile Bwana alivyomwamuru Mose.
4
Hivi ndivyo kinara cha taa kilivyotengenezwa: Kilitengenezwa kwa dhahabu iliyofuliwa, kuanzia kwenye kitako chake hadi kwenye maua yake. Kinara cha taa kilitengenezwa sawasawa kabisa na kielelezo ambacho Bwana alikuwa amemwonyesha Mose.
5
Bwana akamwambia Mose:
6
“Watwae Walawi kutoka miongoni mwa Waisraeli wengine na uwatakase kwa kawaida ya ibada.
7
Ili kuwatakasa fanya hivi: Nyunyizia maji ya utakaso juu yao; kisha uwaambie wanyoe nywele kwenye mwili mzima, wafue nguo zao na hivyo wajitakase wenyewe.
8
Waambie wamchukue fahali mchanga pamoja na sadaka yake ya nafaka ya unga laini uliochanganywa na mafuta; kisha utamchukua fahali mchanga wa pili kwa ajili ya sadaka ya dhambi.
9
Walete Walawi mbele ya Hema la Kukutania na ukusanye jumuiya yote ya Waisraeli.
10
Utawaleta Walawi mbele za Bwana, na Waisraeli wataweka mikono yao juu ya Walawi.
11
Aroni atawaweka Walawi mbele za Bwana kama sadaka ya kuinua kutoka kwa Waisraeli, ili kwamba wawe tayari kuifanya kazi ya Bwana.
12
“Baada ya Walawi kuweka mikono yao juu ya vichwa vya hao mafahali wawili, tumia mmoja kwa ajili ya sadaka ya dhambi kwa Bwana, na mwingine kuwa sadaka ya kuteketezwa, ili kufanya upatanisho kwa ajili ya Walawi.
13
Waambie hao Walawi wasimame mbele ya Aroni na wanawe, kisha wawatoe kama sadaka ya kuinuliwa kwa Bwana.
14
Kwa njia hii utakuwa umewatenga Walawi kutoka kwa Waisraeli wengine, nao Walawi watakuwa wangu.
15
“Utakapokuwa umekwisha kuwatakasa Walawi na kuwatoa kama sadaka ya kuinuliwa, watakuja kufanya kazi yao katika Hema la Kukutania.
Maandiko ya Biblia: Biblica® Open Kiswahili Contemporary Version (Neno: Bibilia Takatifu)™, © 1984, 1989, 2009, 2015 Biblica, Inc. · CC BY-SA 4.0“Biblica” is a trademark registered in the United States Patent and Trademark Office by Biblica, Inc., used with permission.
Settings