Walawi 8:14-23
14
Kisha akamtoa fahali kwa ajili ya sadaka ya dhambi, nao Aroni na wanawe wakaweka mikono yao juu ya kichwa chake.
15
Mose akamchinja yule fahali na akachukua sehemu ya hiyo damu, kisha kwa kidole chake akaitia kwenye pembe zote za madhabahu ili kutakasa madhabahu. Akaimwaga damu iliyobaki chini ya madhabahu. Kwa hiyo akayaweka wakfu ili kufanya upatanisho kwa ajili ya madhabahu.
16
Pia Mose akachukua mafuta yote yanayozunguka sehemu za ndani, mafuta yanayofunika ini, figo zote mbili pamoja na mafuta yake, akayateketeza juu ya madhabahu.
17
Lakini fahali, ikiwa pamoja na ngozi yake na nyama yake na sehemu zake za ndani na matumbo, akaiteketeza nje ya kambi, kama Bwana alivyomwagiza Mose.
18
Kisha Mose akamleta kondoo dume kwa ajili ya sadaka ya kuteketezwa, naye Aroni na wanawe wakaweka mikono yao juu ya kichwa chake.
19
Ndipo Mose akamchinja yule kondoo dume na kunyunyiza damu yake pande zote za madhabahu.
20
Mose akamkata yule kondoo dume vipande vipande na kukiteketeza kichwa, vile vipande na yale mafuta.
21
Kisha akamsafisha sehemu za ndani na miguu kwa maji, na kumteketeza yule kondoo dume mzima juu ya madhabahu kuwa sadaka ya kuteketezwa, harufu nzuri ya kupendeza, sadaka iliyotolewa kwa Bwana kwa moto, kama Bwana alivyomwagiza Mose.
22
Kisha akaleta kondoo dume mwingine, ndiye kondoo dume kwa ajili ya kuwaweka wakfu, naye Aroni na wanawe wakaweka mikono yao juu ya kichwa chake.
23
Mose akamchinja yule kondoo dume, akaichukua sehemu ya damu yake na kuipaka juu ya ncha ya sikio la kuume la Aroni, na juu ya kidole gumba cha mkono wake wa kuume na juu ya kidole kikubwa cha mguu wake wa kuume.
Settings