Walawi 19:1-16
1
Bwana akamwambia Mose,
2
“Sema na kusanyiko lote la Israeli na uwaambie: ‘Kuweni watakatifu, kwa kuwa mimi, Bwana Mungu wenu, ni mtakatifu.
3
“ ‘Kila mmoja wenu ni lazima amheshimu mama yake na baba yake, na pia ni lazima kuzishika Sabato zangu. Mimi ndimi Bwana Mungu wenu.
4
“ ‘Msiabudu sanamu, wala msijitengenezee miungu ya shaba. Mimi ndimi Bwana Mungu wenu.
5
“ ‘Mnapotoa dhabihu ya sadaka ya amani kwa Bwana, toeni kwa namna ambayo itakubaliwa kwa niaba yenu.
6
Sadaka hiyo italiwa siku iyo hiyo mnayoitoa, au kesho yake; chochote kitakachobaki hadi siku ya tatu lazima kiteketezwe kwa moto.
7
Kama sehemu yoyote ya sadaka hiyo italiwa siku ya tatu, itakuwa si safi, nayo haitakubaliwa.
8
Yeyote atakayekula atawajibishwa, kwa sababu amenajisi kitu kilicho kitakatifu kwa Bwana; mtu huyo lazima akatiliwe mbali na watu wake.
9
“ ‘Wakati uvunapo mavuno ya nchi yako, usivune hadi kwenye mipaka ya shamba lako, wala usikusanye mabaki ya mavuno yako.
10
Usirudi mara ya pili katika shamba lako la mizabibu, wala usiokote zabibu zilizoanguka chini. Ziache kwa ajili ya maskini na mgeni. Mimi ndimi Bwana Mungu wako.
11
“ ‘Usiibe. “ ‘Usiseme uongo. “ ‘Msidanganyane.
12
“ ‘Usiape kwa uongo kwa Jina langu, na hivyo kulinajisi jina la Mungu wako. Mimi ndimi Bwana.
13
“ ‘Usimdhulumu wala kumwibia jirani yako. “ ‘Usishikilie mshahara wa kibarua usiku kucha hadi asubuhi.
14
“ ‘Usimlaani kiziwi, wala usiweke kikwazo mbele ya kipofu, lakini umche Mungu wako. Mimi ndimi Bwana.
15
“ ‘Usipotoshe haki; usionyeshe kumpendelea maskini, wala upendeleo kwa mwenye cheo, bali mwamulie jirani yako kwa haki.
16
“ ‘Usieneze uchochezi miongoni mwa watu wako. “ ‘Usifanye kitu chochote kile kinachohatarisha maisha ya jirani yako. Mimi ndimi Bwana.
Maandiko ya Biblia: Biblica® Open Kiswahili Contemporary Version (Neno: Bibilia Takatifu)™, © 1984, 1989, 2009, 2015 Biblica, Inc. · CC BY-SA 4.0“Biblica” is a trademark registered in the United States Patent and Trademark Office by Biblica, Inc., used with permission.
Settings