Walawi 15:16-28
16
“ ‘Wakati mtu akitokwa na shahawa, ni lazima aoge mwili mzima kwa maji, na atakuwa najisi mpaka jioni.
17
Vazi lolote ama ngozi yoyote yenye shahawa juu yake ni lazima ioshwe kwa maji, na itakuwa najisi mpaka jioni.
18
Ikiwa mtu atalala na mwanamke, na kukawa na kutoka kwa shahawa, ni lazima wote waoge kwa maji, nao watakuwa najisi mpaka jioni.
19
“ ‘Ikiwa mwanamke atatokwa na damu ya kawaida ya mwezi, atakuwa najisi kwa siku saba, na yeyote atakayemgusa atakuwa najisi mpaka jioni.
20
“ ‘Chochote atakacholalia wakati wake wa hedhi kitakuwa najisi, na chochote atakachokikalia kitakuwa najisi.
21
Yeyote atakayegusa kitanda chake ni lazima afue nguo zake na aoge kwa maji, naye atakuwa najisi mpaka jioni.
22
Yeyote atakayegusa chochote atakachokalia ni lazima afue nguo zake na aoge kwa maji, naye atakuwa najisi mpaka jioni.
23
Kiwe ni kitanda ama chochote alichokuwa amekikalia, ikiwa mtu yeyote atakigusa, atakuwa najisi mpaka jioni.
24
“ ‘Ikiwa mwanaume atalala naye na ile damu ya mwezi ikamgusa, atakuwa najisi kwa siku saba; kitanda chochote atakachokilalia huyo mwanaume kitakuwa najisi.
25
“ ‘Ikiwa mwanamke atatokwa na damu kwa siku nyingi zaidi ya siku zake za mwezi, au amekuwa na damu inayoendelea zaidi ya kipindi chake, atakuwa najisi kwa kipindi chote cha shida hiyo, kama ilivyokuwa katika siku za hedhi yake.
26
Kitanda chochote atakachokilalia huyo mwanamke wakati anaendelea kutokwa na damu kitakuwa najisi, kama kilivyokuwa kitanda chake wakati wa siku zake za hedhi, na chochote atakachokalia kitakuwa najisi, kama wakati wake wa hedhi.
27
Yeyote agusaye vitu hivyo atakuwa najisi; ni lazima afue nguo zake na kuoga kwa maji, naye atakuwa najisi mpaka jioni.
28
“ ‘Wakati atakapotakasika kutoka hedhi yake, ni lazima ahesabu siku saba, na baada ya hapo atakuwa safi kwa kawaida ya ibada.
Settings