Skip to content
Walawi 14:10-32

Walawi 14:10-32

10
“Siku ya nane, ni lazima alete kondoo dume wawili na kondoo jike mmoja, wote wa mwaka mmoja na wasio na dosari, pamoja na sehemu tatu za kumi za efa za unga laini uliochanganywa na mafuta, kwa ajili ya sadaka ya nafaka, na logi moja ya mafuta.
11
Kuhani atakayemtangaza kuwa safi atahitaji kumkabidhi mgonjwa aliyepona pamoja na sadaka zake zote mbele za Bwana katika ingilio la Hema la Kukutania.
12
“Kisha kuhani atamchukua mmoja wa wale kondoo dume na kumtoa kuwa sadaka ya hatia, pamoja na ile logi moja ya mafuta; ataviinua mbele za Bwana kuwa sadaka ya kuinuliwa.
13
Atamchinja huyo kondoo katika mahali patakatifu ambapo sadaka ya dhambi na ile ya kuteketezwa huchinjiwa. Kama ilivyo sadaka ya dhambi, sadaka ya hatia ni ya kuhani; nayo ni takatifu sana.
14
Kuhani atachukua sehemu ya damu ya sadaka ya hatia na kuitia kwenye ncha ya sikio la kuume la yule atakayetakaswa, kwenye kidole gumba cha mkono wake wa kuume, na kidole kikubwa cha mguu wake wa kuume.
15
Kuhani atachukua sehemu ya ile logi ya mafuta, ayamimine kwenye kiganja cha mkono wake mwenyewe wa kushoto,
16
na achovye kidole chake cha shahada cha mkono wake wa kuume kwenye mafuta yaliyoko kwenye kiganja chake, na kwa kidole hicho anyunyize mafuta hayo mara saba mbele za Bwana.
17
Kuhani atampaka yule anayetakaswa sehemu ya mafuta yaliyobaki kiganjani kwenye ncha ya sikio lake la kuume, kwenye kidole gumba cha mkono wake wa kuume, na kidole kikubwa cha mguu wake wa kuume, mahali palepale alipompaka damu ya sadaka ya kuondoa hatia.
18
Kuhani atayapaka mafuta yaliyobaki kwenye kiganja chake juu ya kichwa cha yule anayetakaswa, na kufanya upatanisho kwa ajili yake mbele za Bwana.
19
“Kisha kuhani atatoa dhabihu ya sadaka ya dhambi na kufanya upatanisho kwa ajili ya yule atakayetakaswa kutoka unajisi wake. Baada ya hayo, kuhani atachinja sadaka ya kuteketezwa
20
na kuitoa juu ya madhabahu, pamoja na sadaka ya nafaka ili kumfanyia upatanisho, naye atakuwa safi.
21
“Hata hivyo, kama ni maskini na hawezi kupata vitu hivi, lazima achukue mwana-kondoo mmoja kama sadaka ya hatia ipate kuinuliwa ili kumfanyia upatanisho, pamoja na sehemu ya kumi ya efa ya unga laini uliochanganywa na logi moja ya mafuta kwa ajili ya sadaka ya nafaka,
22
na hua wawili au makinda mawili ya njiwa, kile atakachoweza kupata, mmoja kwa sadaka ya dhambi, na mwingine kwa sadaka ya kuteketezwa.
23
“Katika siku ya nane, lazima avilete vitu hivyo kwa kuhani, kwa ajili ya kutakaswa kwake kwenye ingilio la Hema la Kukutania mbele za Bwana.
24
Kuhani atamchukua mwana-kondoo kwa ajili ya sadaka ya hatia, pamoja na ile logi ya mafuta ya kuinuliwa mbele za Bwana kuwa sadaka ya kuinuliwa.
25
Atamchinja huyo mwana-kondoo kwa ajili ya sadaka ya hatia. Pia ataichukua sehemu ya damu yake na kuipaka kwenye ncha ya sikio la kuume la yule anayetakaswa, na aipake pia kwenye kidole gumba cha mkono wa kuume wa huyo mtu, na kidole kikubwa cha mguu wake wa kuume.
26
Kuhani atamiminia sehemu ya mafuta kwenye kiganja chake cha mkono wa kushoto,
27
na kwa kidole chake cha shahada cha mkono wa kuume, atamnyunyizia yule anayetakaswa yale mafuta yaliyo kwenye kiganja chake mara saba mbele za Bwana.
28
Atampaka mafuta yaliyobaki kwenye kiganja chake katika sehemu zote, kama alivyompaka damu ya sadaka ya hatia: yaani, kwenye ncha ya sikio la kuume la yule anayetakaswa, kwenye kidole gumba cha mkono wake wa kuume, na kidole kikubwa cha mguu wake wa kuume.
29
Kuhani atayapaka mafuta yaliyobaki katika kiganja chake kwenye kichwa cha yule anayetakaswa, na kufanya upatanisho kwa ajili yake mbele za Bwana.
30
Kisha atatoa dhabihu wale hua ama yale makinda ya njiwa ambayo mtu ataweza kuwapata,
31
mmoja kwa ajili ya sadaka ya dhambi, na mwingine kuwa sadaka ya kuteketezwa, pamoja na sadaka ya nafaka. Kwa njia hii kuhani atafanya upatanisho mbele za Bwana kwa ajili ya yule anayetakaswa.”
32
Haya ndiyo masharti kwa mtu yeyote mwenye ugonjwa wa ngozi wa kuambukiza, na ambaye hana uwezo wa kutoa sadaka za kawaida kwa ajili ya kutakaswa kwake.
Settings

Reading Style

Typeface

Font Size 19px

Options