Waamuzi 9:26-41
26
Basi Gaali mwana wa Ebedi akaenda pamoja na ndugu zake wakaingia Shekemu, nao watu wa huko wakamtumainia yeye.
27
Wakaenda mashambani mwao kuvuna zabibu na kuzisindika hizo zabibu, wakafanya sikukuu katika hekalu la mungu wao. Wakati wakila na kunywa, wakamlaani Abimeleki.
28
Gaali mwana wa Ebedi akasema, “Abimeleki ni nani, na Shekemu ni nani, hata tumtumikie? Je, yeye si mwana wa Yerub-Baali? Naye Zebuli si ndiye msaidizi wake? Basi watumikieni watu wa Hamori, babaye Shekemu. Kwa nini tumtumikie Abimeleki?
29
Laiti watu hawa wangekuwa chini ya amri yangu! Basi mimi ningemwondoa huyo Abimeleki. Ningemwambia Abimeleki, ‘Ondoa jeshi lako lote.’ ”
30
Zebuli aliyekuwa mtawala wa mji aliposikia aliyosema Gaali mwana wa Ebedi, akakasirika sana.
31
Akatuma ujumbe uende kwa Abimeleki kwa siri na kusema, “Gaali mwana wa Ebedi na ndugu zake wamekuja Shekemu, na wanauchochea mji huu kinyume chako.
32
Sasa, basi, usiku huu wewe uondoke na watu wako ili mje kuwavizia mashambani.
33
Kisha asubuhi wakati wa kuchomoza jua, amka mapema na ujipange dhidi ya huo mji. Wakati yeye na jeshi lililo pamoja naye watakapotoka kukabiliana nanyi, mwaweza kuwatendea kwa kadiri mnavyoweza.”
34
Kwa hiyo Abimeleki pamoja na jeshi lake lote wakaondoka usiku na kujificha karibu na Shekemu wakiwa vikosi vinne.
35
Basi Gaali mwana wa Ebedi alikuwa ametoka nje akawa amesimama katika ingilio la mji wakati ule ule ambao Abimeleki na watu wake walipokuwa wanatoka sehemu zao za maficho.
36
Gaali alipowaona, akamwambia Zebuli, “Tazama, watu wanashuka kutoka kwenye vilele vya milima!” Zebuli akajibu, “Wewe unaona vivuli vya milima kana kwamba ni watu.”
37
Lakini Gaali akasema tena, “Tazama, watu wanashuka kutoka katikati ya nchi na kikosi kimoja kinakuja kutoka Tabur-Ezeri na kikosi kingine kutoka upande wa Elon-Meonenimu.”
38
Ndipo Zebuli akamwambia, “Kuko wapi kujivuna kwako sasa, wewe uliyesema, ‘Huyo Abimeleki ni nani hata tumtumikie?’ Hawa si wale watu uliowadharau? Toka nje sasa ukapigane nao!”
39
Basi Gaali akatoka akawaongoza watu wa Shekemu kupigana na Abimeleki.
40
Abimeleki akamfukuza, watu wengi wakajeruhiwa katika kukimbia huko, njia nzima hadi kwenye ingilio la lango.
41
Abimeleki akakaa Aruma, naye Zebuli akawafukuza Gaali na ndugu zake watoke Shekemu.
Settings