Ayubu 33:14-30
14
Kwa kuwa Mungu husema, wakati huu kwa njia moja, au wakati mwingine kwa njia nyingine, ingawa mwanadamu anaweza asielewe.
15
Mungu husema na mwanadamu katika ndoto, katika maono ya usiku, wakati usingizi mzito uwaangukiapo wanadamu wasinziapo vitandani mwao,
16
anaweza akasemea masikioni mwao, na kuwatia hofu kwa maonyo,
17
ili kumgeuza mtu kutoka kwenye kutenda mabaya na kumwepusha na kiburi,
18
kuiokoa nafsi yake na shimo, uhai wake usiangamizwe kwa upanga.
19
Mtu anaweza kutiwa adabu kwa maumivu kitandani mwake, kwa dhiki za mfululizo katika mifupa yake,
20
kiasi kwamba maisha yake yenyewe yanakataa chakula nayo nafsi yake ikakichukia kabisa hata chakula kizuri.
21
Nyama ya mwili wake huisha kwa kukonda, nayo mifupa yake ambayo mwanzoni ilikuwa imefichika, sasa inatokeza nje.
22
Nafsi yake inakaribia kaburi, nao uhai wake karibu na wajumbe wa kifo.
23
“Kama bado kuna malaika upande wake kama mtetezi, mmoja miongoni mwa elfu, wa kumwambia mwanadamu lililo jema kwake,
24
kumwonea huruma na kusema, ‘Mwokoe asije akatumbukia shimoni; nimepata ukombozi kwa ajili yake’:
25
ndipo nyama ya mwili wake hufanywa mpya kama ya mtoto; hurudishwa upya kama siku za ujana wake.
26
Humwomba Mungu, akapata kibali kwake, huuona uso wa Mungu na kushangilia kwa furaha; Mungu humrudisha katika hali yake ya uadilifu.
27
Ndipo huja mbele za watu na kusema, ‘Nilitenda dhambi na kupotosha kilichokuwa haki, lakini sikuadhibiwa kama nilivyostahili.
28
Alinikomboa nafsi yangu nisitumbukie shimoni, nami nitaishi ili kuufurahia mwanga.’
29
“Mungu hufanya haya yote kwa mwanadamu; mara mbili hata mara tatu,
30
ili aigeuze nafsi yake toka shimoni, ili nuru ya uzima imwangazie.
Settings