Yeremia 51:6-14
6
“Kimbieni kutoka Babeli! Okoeni maisha yenu! Msiangamizwe kwa sababu ya dhambi zake. Ni wakati wa kisasi cha Bwana, atamlipa kile anachostahili.
7
Babeli alikuwa kikombe cha dhahabu katika mkono wa Bwana; aliufanya ulimwengu wote ulewe. Mataifa walikunywa mvinyo wake; kwa hiyo sasa wameingiwa na wazimu.
8
Babeli ataanguka ghafula na kuvunjika. Mwombolezeni! Tafuteni zeri ya kutuliza maumivu yake, labda anaweza kupona.
9
“ ‘Tungemponya Babeli, lakini hawezi kuponyeka; tumwacheni, na kila mmoja wetu aende nchi yake mwenyewe, kwa kuwa hukumu yake inafika angani, inapanda juu hadi mawinguni.’
10
“ ‘Bwana amethibitisha haki yetu; njooni, tutangaze katika Sayuni kitu ambacho Bwana Mungu wetu amefanya.’
11
“Noeni mishale, chukueni ngao! Bwana amewaamsha wafalme wa Wamedi, kwa sababu nia yake ni kuangamiza Babeli. Bwana atalipiza kisasi, kisasi kwa ajili ya Hekalu lake.
12
Twekeni bendera juu ya kuta za Babeli! Imarisheni ulinzi, wekeni walinzi, andaeni waviziao! Bwana atatimiza kusudi lake, amri yake juu ya watu wa Babeli.
13
Wewe uishiye kando ya maji mengi na uliye na wingi wa hazina, mwisho wako umekuja, wakati wako wa kukatiliwa mbali.
14
Bwana Mwenye Nguvu Zote ameapa kwa nafsi yake mwenyewe: ‘Hakika nitakujaza na watu, kama kundi la nzige, nao watapiga kelele za ushindi juu yako.’
Settings