Yeremia 51:34-44
34
“Nebukadneza mfalme wa Babeli ametula, ametufanya tuchangayikiwe, ametufanya tuwe gudulia tupu. Kama nyoka ametumeza na kujaza tumbo lake kwa vyakula vyetu vizuri, kisha akatutapika.
35
Jeuri iliyofanyiwa miili yetu na iwe juu ya Babeli,” ndivyo wasemavyo wakaao Sayuni. “Damu yetu na iwe juu ya wale waishio Babeli,” asema Yerusalemu.
36
Kwa hiyo, hili ndilo Bwana asemalo: “Tazama, nitatetea shauri lako na kulipiza kisasi kwa ajili yako; nitaikausha bahari yake na kuzikausha chemchemi zake.
37
Babeli utakuwa lundo la magofu na makao ya mbweha, kitu cha kutisha na kudharauliwa, mahali asipoishi mtu.
38
Watu wake wote wananguruma kama simba wadogo, wanakoroma kama wana simba.
39
Lakini wakati wakiwa wameamshwa, nitawaandalia karamu na kuwafanya walewe, ili wapige kelele kwa kicheko, kisha walale milele na wasiamke,” asema Bwana.
40
“Nitawateremsha kama wana-kondoo waendao machinjoni, kama kondoo dume na mbuzi.
41
“Tazama jinsi Sheshaki atakamatwa, majivuno ya dunia yote yatakavyonyakuliwa. Babeli atakuwa mwenye hofu kiasi gani kati ya mataifa!
42
Bahari itainuka juu ya Babeli; mawimbi yake yenye kunguruma yatamfunika.
43
Miji yake itakuwa ukiwa, kame na jangwa, nchi ambayo hakuna yeyote anayeishi ndani yake, ambayo hakuna mtu anayepita humo.
44
Nitamwadhibu Beli katika Babeli, na kumfanya atapike kile alichokimeza. Mataifa hayatamiminika tena kwake. Nao ukuta wa Babeli utaanguka.
Settings