Skip to content
Yeremia 36:10-26

Yeremia 36:10-26

10
Kutoka chumba cha Gemaria mwana wa Shafani mwandishi, kilichokuwa katika ua wa juu kwenye ingilio la Lango Jipya la Hekalu, Baruku akawasomea watu wote waliokuwa katika Hekalu la Bwana maneno ya Yeremia kutoka kwenye kile kitabu.
11
Basi Mikaya mwana wa Gemaria, mwana wa Shafani, aliposikia maneno yote ya Bwana kutoka kwenye kile kitabu,
12
alishuka hadi kwenye chumba cha mwandishi kwenye jumba la kifalme, mahali walipokuwa wameketi maafisa wote: yaani Elishama mwandishi, Delaya mwana wa Shemaya, Elnathani mwana wa Akbori, Gemaria mwana wa Shafani, Sedekia mwana wa Hanania, na maafisa wengine wote.
13
Baada ya Mikaya kuwaambia kila kitu ambacho alikuwa amesikia Baruku akiwasomea watu kutoka kwenye kile kitabu,
14
maafisa wote wakamtuma Yehudi mwana wa Nethania, mwana wa Shelemia, mwana wa Kushi, kumwambia Baruku, “Leta hicho kitabu ambacho umewasomea watu, nawe mwenyewe uje.” Ndipo Baruku mwana wa Neria akawaendea akiwa na hicho kitabu mkononi mwake.
15
Wakamwambia, “Tafadhali, keti na utusomee hicho kitabu.” Ndipo Baruku akawasomea kile kitabu.
16
Walipoyasikia maneno hayo yote, wakatazamana wao kwa wao kwa woga na kumwambia Baruku, “Lazima tutoe taarifa ya maneno haya yote kwa mfalme.”
17
Kisha wakamuuliza Baruku, “Tuambie, uliandikaje haya yote? Je, yalitoka kinywani mwa Yeremia?”
18
Baruku akajibu, “Ndiyo, maneno haya yote yalitoka kinywani mwa Yeremia, nami nikayaandika kwa wino katika hiki kitabu.”
19
Ndipo wale maafisa wakamwambia Baruku, “Wewe na Yeremia nendeni mkajifiche. Mtu yeyote asijue mahali mlipo.”
20
Baada ya kuhifadhi kile kitabu ndani ya chumba cha Elishama mwandishi, wakamwendea mfalme katika ua wa nje na kumwarifu kila kitu.
21
Mfalme akamtuma Yehudi akachukue kile kitabu. Yehudi akakileta hicho kitabu kutoka kwenye chumba cha Elishama mwandishi, na akakisoma mbele ya mfalme na maafisa wakiwa wamesimama kando ya mfalme.
22
Ulikuwa mwezi wa tisa, na mfalme alikuwa ameketi chumba cha wakati wa baridi akiota moto.
23
Hata ikawa kila wakati Yehudi alipomaliza kusoma kurasa tatu au nne za hicho kitabu, mfalme alizikata kwa kisu cha mwandishi na kuzitupia motoni, hadi kitabu chote kikateketea.
24
Mfalme na watumishi wake wote waliosikia yote yaliyosomwa hawakuonyesha hofu yoyote, wala hawakuyararua mavazi yao.
25
Hata ingawa Elnathani, Delaya na Gemaria walimsihi mfalme asikichome kile kitabu, yeye hakuwasikiliza.
26
Badala yake, mfalme akamwamuru Yerameeli, mwana wa mfalme, Seraya mwana wa Azrieli, na Shelemia mwana wa Abdeeli kuwakamata mwandishi Baruku na nabii Yeremia. Lakini Bwana alikuwa amewaficha.
Settings

Reading Style

Typeface

Font Size 19px

Options