Yeremia 35:12-17
12
Ndipo neno la Bwana likamjia Yeremia kusema:
13
“Hili ndilo Bwana Mwenye Nguvu Zote, aliye Mungu wa Israeli, asemalo: Nenda ukawaambie watu wa Yuda na watu wa Yerusalemu, ‘Je, hamwezi kujifunza kutoka kwa wana wa Rekabu, na kuyatii maneno yangu?’ asema Bwana.
14
‘Yonadabu mwana wa Rekabu aliwaagiza wanawe wasinywe divai, na agizo hilo wamelishika mpaka leo hawanywi divai, kwa sababu wanatii amri ya baba yao. Lakini nimenena nanyi tena na tena, lakini hamkunitii mimi.
15
Tena na tena nimewatuma watumishi wangu wote manabii kwenu. Wakasema, “Kila mmoja wenu ni lazima ageuke na kuacha njia zake mbaya, na kuyatengeneza matendo yake. Msifuate miungu mingine ili kuitumikia. Ndipo mtakapoishi katika nchi niliyowapa ninyi na baba zenu.” Lakini hamkujali wala kunisikiliza.
16
Wazao wa Yonadabu mwana wa Rekabu walitimiza amri ambayo baba yao aliwapa, lakini watu hawa hawakunitii mimi.’
17
“Kwa hiyo, hili ndilo Bwana Mungu Mwenye Nguvu Zote, Mungu wa Israeli, asemalo: ‘Sikilizeni! Nitaleta juu ya Yuda na juu ya kila mmoja aishiye Yerusalemu kila aina ya maafa niliyotamka dhidi yao. Nilinena nao, lakini hawakusikiliza. Niliwaita, lakini hawakujibu.’ ”
Settings