Yeremia 35:1-11
1
Hili ndilo neno lililomjia Yeremia kutoka kwa Bwana, wakati wa utawala wa Yehoyakimu mwana wa Yosia mfalme wa Yuda:
2
“Nenda kwa jamaa ya Warekabi, uwaalike waje kwenye moja ya vyumba vya pembeni vya nyumba ya Bwana, na uwape divai wanywe.”
3
Basi nikaenda kumwita Yaazania mwana wa Yeremia, mwana wa Habazinia, na ndugu zake na wanawe wote, yaani jamaa nzima ya Warekabi.
4
Nikawaleta katika nyumba ya Bwana, ndani ya chumba cha wana wa Hanani mwana wa Igdalia mtu wa Mungu. Kilikuwa karibu na chumba cha maafisa, ambacho kilikuwa juu ya kile cha Maaseya mwana wa Shalumu, aliyekuwa bawabu.
5
Kisha nikaweka mabakuli yaliyojaa divai na baadhi ya vikombe mbele ya watu wa jamaa ya Warekabi na kuwaambia, “Kunyweni divai.”
6
Lakini wao wakajibu, “Sisi hatunywi divai, kwa sababu baba yetu Yonadabu mwana wa Rekabu, alitupa agizo hili: ‘Ninyi wala wazao wenu kamwe msinywe divai.
7
Pia msijenge nyumba kamwe, wala kuotesha mbegu au kupanda mashamba ya mizabibu. Kamwe msiwe na kitu chochote katika hivi, lakini siku zote lazima muishi kwenye mahema. Ndipo mtakapoishi kwa muda mrefu katika nchi ambayo ninyi ni wahamiaji.’
8
Tumetii kila kitu ambacho baba yetu Yonadabu mwana wa Rekabu alituamuru. Sisi wenyewe wala wake zetu wala wana wetu na binti zetu kamwe hatujanywa divai
9
wala kujenga nyumba za kuishi au kuwa na mashamba ya mizabibu, mashamba au mazao.
10
Tumeishi katika mahema na tumetii kikamilifu kila kitu alichotuamuru baba yetu Yonadabu.
11
Lakini wakati Nebukadneza mfalme wa Babeli alipoivamia nchi hii, tulisema, ‘Njooni, lazima twende Yerusalemu ili kukimbia majeshi ya Wakaldayo na ya Washamu.’ Kwa hiyo tumeishi Yerusalemu.”
Settings