Skip to content
Yeremia 32:1-8

Yeremia 32:1-8

1
Hili ndilo neno lililomjia Yeremia kutoka kwa Bwana, katika mwaka wa kumi wa utawala wa Sedekia mfalme wa Yuda, ambao ulikuwa mwaka wa kumi na nane wa utawala wa Mfalme Nebukadneza.
2
Wakati huo jeshi la mfalme wa Babeli lilikuwa limeuzunguka mji wa Yerusalemu, naye nabii Yeremia alikuwa amezuiliwa katika ua wa walinzi katika jumba la kifalme la Yuda.
3
Basi Sedekia mfalme wa Yuda alikuwa amemfunga huko akisema, “Kwa nini unatabiri hivyo? Wewe unasema, ‘Hili ndilo asemalo Bwana: Ninakaribia kuutia mji huu mkononi mwa mfalme wa Babeli, naye atauteka.
4
Sedekia mfalme wa Yuda hataweza kuponyoka mikononi mwa Wakaldayo, lakini kwa hakika atatiwa mikononi mwa mfalme wa Babeli, naye atazungumza naye ana kwa ana na kumwona kwa macho yake mwenyewe.
5
Atamchukua Sedekia hadi Babeli, mahali atakapoishi mpaka nitakapomshughulikia, asema Bwana. Kama utapigana dhidi ya Wakaldayo, hutashinda.’ ”
6
Yeremia akasema, “Neno la Bwana lilinijia kusema:
7
Hanameli mwana wa Shalumu mjomba wako atakuja kwako na kusema, ‘Nunua shamba langu huko Anathothi, kwa sababu wewe kama jamaa ya karibu ni haki na wajibu wako kulinunua.’
8
“Kisha, kama Bwana alivyosema, binamu yangu Hanameli alinijia katika ua wa walinzi na kusema: ‘Nunua shamba langu lililoko Anathothi katika nchi ya Benyamini. Kwa kuwa ni haki yako kulikomboa na kulimiliki, jinunulie.’ “Nilijua kwamba hili lilikuwa neno la Bwana.
Settings

Reading Style

Typeface

Font Size 19px

Options