Yeremia 31:1-9
1
“Wakati huo, nitakuwa Mungu wa koo zote za Israeli nao watakuwa watu wangu,” asema Bwana.
2
Hili ndilo asemalo Bwana: “Watu watakaopona upanga watapata upendeleo jangwani; nitakuja niwape Israeli pumziko.”
3
Bwana alitutokea wakati uliopita, akisema: “Nimekupenda kwa upendo wa milele, nimekuvuta kwa wema.
4
Nitakujenga tena nawe utajengeka upya, ewe Bikira Israeli. Utachukua tena matari yako na kwenda kucheza na wenye furaha.
5
Utapanda tena shamba la mizabibu juu ya vilima vya Samaria, wakulima watapanda na kufurahia matunda yake.
6
Itakuja siku wakati walinzi watakapowapigia kelele juu ya vilima vya Efraimu wakisema, ‘Njooni, twendeni juu Sayuni, kwake Bwana Mungu wetu.’ ”
7
Hili ndilo asemalo Bwana: “Mwimbieni Yakobo kwa furaha, mpigieni kelele aliye mkuu wa mataifa. Zifanyeni sifa zenu zisikike, nanyi mseme, ‘Ee Bwana, okoa watu wako, mabaki ya Israeli.’
8
Tazama, nitawaleta kutoka nchi ya kaskazini na kuwakusanya kutoka miisho ya dunia. Miongoni mwao watakuwepo vipofu na viwete, mama wajawazito na wenye utungu wa kuzaa. Umati mkubwa wa watu utarudi.
9
Watakuja wakilia; wataomba wakati ninawarudisha. Nitawaongoza kando ya vijito vya maji katika mapito yaliyo tambarare ambapo hawatajikwaa, kwa sababu mimi ndimi baba wa Israeli, naye Efraimu ni mzaliwa wangu wa kwanza.
Settings