Ezekieli 45:7-17
7
“ ‘Mkuu anayetawala atakuwa na lile eneo linalopakana na lile eneo lililowekwa wakfu upande huu na upande huu na eneo la mji. Eneo la mji litaenea upande wa magharibi kuanzia upande wa magharibi na upande wa mashariki kuanzia upande wa mashariki, likiendelea kwa urefu kutoka magharibi hadi mpaka wa mashariki sambamba na mojawapo ya sehemu za makabila.
8
Nchi hii itakuwa milki yake katika Israeli. Nao wakuu wangu hawataonea tena watu wangu bali watairuhusu nyumba ya Israeli kuimiliki nchi kulingana na makabila yao.
9
“ ‘Hili ndilo Bwana Mwenyezi asemalo: Yatosha, enyi wakuu wa Israeli! Acheni mbali ukatili wenu na uonevu wenu mkafanye lile lililo haki na sawa. Acheni kuwatoza watu wangu isivyo haki, asema Bwana Mwenyezi.
10
Tumieni mizani sahihi na vipimo sahihi vya efa na bathi.
11
Efa na bathi viwe sawa, bathi iwe sehemu ya kumi ya homeri na efa iwe sehemu ya kumi ya homeri, homeri itakuwa ndicho kiwango cha kukubalika kwa vyote viwili.
12
Shekeli moja itakuwa gera ishirini. Shekeli ishirini, jumlisha na shekeli ishirini na tano, jumlisha na shekeli kumi na tano zitakuwa mina moja.
13
“ ‘Hili ndilo toleo maalum mtakalotoa: moja ya sita ya efa kutoka kila homeri ya ngano na moja ya sita ya efa kutoka kila homeri ya shayiri.
14
Sehemu ya mafuta iliyoamriwa, yaliyopimwa kwa bathi, ni sehemu ya kumi ya bathi kutoka kila kori moja (ambayo ina bathi kumi au homeri moja.)
15
Pia kondoo mmoja atachukuliwa kutoka kwenye kila kundi la kondoo mia mbili kutoka kwenye malisho yaliyonyeshewa vizuri ya Israeli. Hivi vitatumika kwa ajili ya sadaka ya nafaka, sadaka ya kuteketezwa na sadaka za amani ili kufanya upatanisho kwa ajili ya watu, asema Bwana Mwenyezi.
16
Watu wote wa nchi wataungana pamoja na mkuu anayetawala Israeli ili kutoa hii sadaka maalum.
17
Huu utakuwa ndio wajibu wa mkuu anayetawala kutoa sadaka ya kuteketezwa, sadaka ya nafaka na sadaka ya kinywaji kwenye sikukuu, Mwezi Mwandamo na Sabato, kwenye sikukuu zote zilizoamriwa za nyumba ya Israeli. Atatoa sadaka za dhambi, sadaka za nafaka, sadaka za kuteketezwa na sadaka za amani ili kufanya upatanisho kwa ajili ya nyumba ya Israeli.
Settings