Ezekieli 41:16-26
16
pamoja na vizingiti, madirisha membamba na vyumba vyote vitatu, kila kimoja pamoja na kizingiti vilifunikwa kwa mbao. Sakafu, ukuta mpaka kwenye madirisha na madirisha yenyewe vilifunikwa kwa mbao.
17
Katika nafasi iliyokuwa juu ya upande wa nje wa ingilio la sehemu takatifu ya ndani, na katika kuta zilizozunguka sehemu takatifu ya ndani na sehemu takatifu ya nje, kwa nafasi zilizo sawa,
18
kulinakshiwa makerubi na miti ya mitende. Miti ya mitende ilikuwa kati ya kerubi na kerubi. Kila kerubi alikuwa na nyuso mbili:
19
upande mmoja uso wa mwanadamu kuelekea mti wa mtende na upande mwingine uso wa simba ukielekea mti mwingine wa mtende. Ilinakshiwa kuzunguka Hekalu lote.
20
Kuanzia sakafu mpaka eneo lililo juu ya ingilio, palinakshiwa makerubi na miti ya mitende pamoja na kwenye ukuta wa nje wa patakatifu.
21
Mahali patakatifu pa nje palikuwa na miimo ya mlango uliokuwa mraba na ule uliokuwa katika Patakatifu Pa Patakatifu ulikuwa unafanana na huo mwingine.
22
Kulikuwa na madhabahu ya mbao kimo chake dhiraa tatu na ilikuwa dhiraa mbili mraba pande zote, tako lake na pande zake zilikuwa za mbao. Yule mtu akaniambia, “Hii ni meza ambayo iko mbele za Bwana.”
23
Mahali patakatifu pa nje na Patakatifu Pa Patakatifu zilikuwa na milango miwili.
24
Kila mlango ulikuwa na vipande viwili, vipande viwili vilivyoshikwa na bawaba vyenye kufunguka kwa kila mlango.
25
Juu ya hiyo milango ya Patakatifu palinakshiwa makerubi na miti ya mitende kama yale yaliyonakshiwa kwenye kuta, na kulikuwa na ubao ulioningʼinia mbele ya baraza kwa nje.
26
Katika kuta za pembeni za ukumbi kulikuwa na madirisha membamba yaliyonakshiwa miti ya mitende kila upande. Vyumba vya pembeni vya Hekalu pia vilikuwa vimefunikwa kwa mbao.
Settings