Ezekieli 39:1-11
1
“Mwanadamu, tabiri dhidi ya Gogu useme: ‘Hili ndilo Bwana Mwenyezi asemalo: Ee Gogu mimi ni kinyume nawe, mtawala mkuu wa Roshi, Mesheki na Tubali.
2
Nitakugeuza kuelekea ulikotoka na kukuburuta. Nitakuleta kutoka kaskazini ya mbali na kukupeleka wewe dhidi ya milima ya Israeli.
3
Kisha nitaupiga upinde wako kutoka mkono wako wa kushoto na kuifanya mishale ianguke kutoka mkono wako wa kuume.
4
Utaanguka kwenye milima ya Israeli, wewe pamoja na vikosi vyako vyote na yale mataifa yaliyo pamoja nawe. Nitakutoa uwe chakula cha ndege wa aina zote walao nyama na cha wanyama wa mwituni.
5
Utaanguka katika uwanja, kwa kuwa nimenena, asema Bwana Mwenyezi.
6
Nitatuma moto juu ya Magogu na kwa wale wanaoishi kwa salama huko pwani, nao watajua kwamba Mimi ndimi Bwana.
7
“ ‘Nitalifanya Jina langu takatifu lijulikane miongoni mwa watu wangu Israeli. Sitaliacha tena Jina langu takatifu litiwe unajisi, nayo mataifa watajua kuwa Mimi Bwana ndimi Aliye Mtakatifu wa Israeli.
8
Hili jambo linakuja! Hakika litatokea, asema Bwana Mwenyezi. Hii ndiyo siku ile niliyosema habari zake.
9
“ ‘Ndipo wale wanaoishi katika miji ya Israeli watakapotoka na kutumia hizo silaha kuwashia moto na kuziteketeza, yaani, kigao na ngao, pinde na mishale, rungu za vita na mikuki. Kwa miaka saba watavitumia kama kuni.
10
Hawatahitaji kukusanya kuni kutoka mashambani wala kukata kuni kutoka kwenye misitu, kwa sababu watatumia silaha kuwa kuni. Nao watawateka mateka wale waliowateka na kuchukua nyara mali za wale waliochukua mali zao nyara, asema Bwana Mwenyezi.
11
“ ‘Siku ile nitampa Gogu mahali pa kuzikia katika Israeli, katika bonde la wale wasafirio upande wa mashariki kuelekea baharini. Jambo hili litazuia njia ya wasafiri kwa sababu Gogu na makundi yake yote ya wajeuri watazikwa huko. Kwa hiyo litaitwa Bonde la Hamon-Gogu.
Settings