Ezekieli 29:1-16
1
Katika mwaka wa kumi, mwezi wa kumi, siku ya kumi na mbili, neno la Bwana likanijia kusema:
2
“Mwanadamu, elekeza uso wako juu ya Farao mfalme wa Misri na utabiri dhidi yake na dhidi ya Misri yote.
3
Nena, nawe useme: ‘Hili ndilo Bwana Mwenyezi asemalo: “ ‘Mimi ni kinyume nawe, Farao, mfalme wa Misri, joka kubwa ulalaye katikati ya vijito vyako. Unasema, “Mto Naili ni wangu mwenyewe; niliufanya kwa ajili yangu mwenyewe.”
4
Lakini nitatia ndoana katika mataya yako nami nitawafanya samaki wa vijito vyako washikamane na magamba yako. Nitakutoa katikati ya vijito vyako, pamoja na samaki wote walioshikamana na magamba yako.
5
Nitakutupa jangwani, wewe pamoja na samaki wote wa vijito vyako. Utaanguka uwanjani, nawe hutakusanywa au kuchukuliwa. Nitakutoa uwe chakula kwa wanyama wa nchi na ndege wa angani.
6
Ndipo wale wote waishio Misri watakapojua kuwa Mimi ndimi Bwana. “ ‘Umekuwa fimbo ya tete kwa nyumba ya Israeli.
7
Walipokushika kwa mikono yao, ulivunjika na kuchana mabega yao; walipokuegemea, ulivunjika na migongo yao ikateguka.
8
“ ‘Kwa hiyo hili ndilo Bwana Mwenyezi asemalo: Nitaleta upanga juu yako na kuua watu wako na wanyama wao.
9
Misri itakuwa ukiwa na isiyolimwa wala kukaliwa na watu. Ndipo watakapojua kuwa Mimi ndimi Bwana. “ ‘Kwa sababu ulisema, “Mto Naili ni wangu; mimi niliufanya,”
10
kwa hiyo mimi ni kinyume nawe na kinyume na vijito vyako, nami nitaifanya nchi ya Misri kuwa magofu na ukiwa isiyolimwa wala kukaliwa na watu kuanzia Migdoli hadi Aswani, hata kufikia mpakani wa Ethiopia.
11
Hakuna unyayo wa mtu au mnyama utakaopita ndani yake, wala hakuna yeyote atakayeishi humo kwa muda wa miaka arobaini.
12
Nitaifanya nchi ya Misri ukiwa, miongoni mwa nchi zilizo ukiwa, nayo miji yake itabaki ukiwa miaka arobaini miongoni mwa miji iliyo magofu. Nami nitawatawanya Wamisri miongoni mwa mataifa na kuwafukuza huku na huko katika nchi nyingine.
13
“ ‘Lakini hili ndilo Bwana Mwenyezi asemalo: Mwishoni mwa hiyo miaka arobaini, nitawakusanya Wamisri kutoka mataifa walikotawanywa.
14
Nitawarudisha hao Wamisri kutoka kwenye kutekwa kwao na kuwaweka katika Pathrosi, nchi ya baba zao. Huko watakuwa na ufalme usiokuwa na nguvu.
15
Utakuwa ufalme dhaifu kuliko zote na kamwe Misri haitajikweza tena juu ya mataifa mengine. Nitaufanya ufalme wake dhaifu sana kiasi kwamba kamwe hautatawala tena juu ya mataifa mengine.
16
Misri haitakuwa tena tumaini la watu wa Israeli bali itakuwa kumbukumbu ya dhambi yao kwa kuigeukia kuomba msaada. Ndipo watakapojua kuwa Mimi ndimi Bwana Mwenyezi.’ ”
Settings