Ezekieli 28:12-19
12
“Mwanadamu, mfanyie maombolezo mfalme wa Tiro, nawe umwambie: ‘Hili ndilo Bwana Mwenyezi asemalo: “ ‘Ulikuwa kipeo cha ukamilifu, ukiwa umejaa hekima na mkamilifu katika uzuri.
13
Ulikuwa ndani ya Edeni, bustani ya Mungu; kila kito cha thamani kilikupamba: akiki nyekundu, yakuti manjano na zumaridi, krisolitho, shohamu na yaspi, yakuti samawi, almasi na zabarajadi. Kuwekwa kwa hayo mapambo na kushikizwa kwake kulifanywa kwa dhahabu; siku ile ulipoumbwa yaliandaliwa tayari.
14
Ulitiwa mafuta kuwa kerubi mlinzi, kwa kuwa hivyo ndivyo nilivyokuweka wakfu. Ulikuwa kwenye mlima mtakatifu wa Mungu; ulitembea katikati ya vito vya moto.
15
Ulikuwa mnyofu katika njia zako tangu siku ile ya kuumbwa kwako, hadi uovu ulipoonekana ndani yako.
16
Kutokana na biashara yako iliyoenea, ulijazwa na dhuluma, nawe ukatenda dhambi. Hivyo nilikuondoa kwa aibu kutoka mlima wa Mungu, nami nikakufukuza, ee kerubi mlinzi, kutoka katikati ya vito vya moto.
17
Moyo wako ukawa na kiburi kwa ajili ya uzuri wako, nawe ukaiharibu hekima yako kwa sababu ya fahari yako. Kwa hiyo nikakutupa chini; nimekufanya kioja mbele ya wafalme.
18
Kwa dhambi zako nyingi na biashara yako ya dhuluma, umenajisi mahali pako patakatifu. Kwa hiyo nilifanya moto utoke ndani yako, nao ukakuteketeza, nami nikakufanya majivu juu ya nchi, machoni pa wote waliokuwa wakitazama.
19
Mataifa yote yaliyokujua yanakustajabia; umefikia mwisho wa kutisha na hutakuwepo tena milele.’ ”
Settings