Ezekieli 21:8-17
8
Neno la Bwana likanijia, kusema:
9
“Mwanadamu, tabiri na useme, ‘Hili ndilo Bwana asemalo: “ ‘Upanga, upanga, ulionolewa na kusuguliwa:
10
umenolewa kwa ajili ya mauaji, umesuguliwa ili ungʼae kama umeme wa radi! “ ‘Je, tuifurahie fimbo ya utawala ya mwanangu Yuda? Upanga unaidharau kila fimbo ya namna hiyo.
11
“ ‘Upanga umewekwa tayari ili kusuguliwa, ili upate kushikwa mkononi, umenolewa na kusuguliwa, umewekwa tayari kwa mkono wa muuaji.
12
Piga kelele na uomboleze, ee mwanadamu, kwa kuwa upanga u dhidi ya watu wangu; u dhidi ya wakuu wote wa Israeli. Wametolewa wauawe kwa upanga pamoja na watu wangu. Kwa hiyo pigapiga kifua chako.
13
“ ‘Kwa maana upanga huu umejaribiwa na kuhakikishwa, itakuwaje basi fimbo ya ufalme ya Yuda inayoudharau kama haitakuwepo tena, bali itakuwa imeondolewa kabisa? asema Bwana Mwenyezi.’
14
“Hivyo basi, mwanadamu, tabiri na ukapige makofi. Upanga wako na upige mara mbili, naam, hata mara tatu. Ni upanga wa kuchinja, upanga wa mauaji makuu, ukiwashambulia kutoka kila upande.
15
Ili mioyo ipate kuyeyuka na wanaouawa wawe wengi, nimeweka upanga wa kuchinja kwenye malango yao yote. Lo! Umetengenezwa umetemete kama umeme wa radi, umeshikwa kwa ajili ya kuua.
16
Ee upanga, kata upande wa kuume, kisha upande wa kushoto, mahali popote makali yako yatakapoelekezwa.
17
Mimi nami nitapiga makofi, nayo ghadhabu yangu itapungua. Mimi Bwana nimesema.”
Settings