Kutoka 9:1-15
1
Ndipo Bwana akamwambia Mose, “Nenda kwa Farao ukamwambie, ‘Hili ndilo Bwana, Mungu wa Waebrania asemalo: “Waachie watu wangu waende ili wapate kuniabudu.”
2
Kama ukikataa kuwaachia waende, nawe ukiendelea kuwashikilia,
3
mkono wa Bwana utaleta pigo baya kwa mifugo yako, juu ya farasi wako, punda, ngamia, ngʼombe wako, kondoo na mbuzi.
4
Lakini Bwana ataweka tofauti kati ya mifugo ya Israeli na ile ya Misri, kwamba hakuna mnyama wa Mwisraeli atakayekufa.’ ”
5
Bwana akaweka wakati na kusema, “Kesho Bwana atalitenda hili katika nchi.”
6
Siku iliyofuata Bwana akalitenda: Mifugo yote ya Wamisri ikafa, lakini hakuna hata mnyama mmoja wa wana wa Israeli aliyekufa.
7
Farao akatuma watu kuchunguza, nao wakakuta kuwa hakuna hata mnyama mmoja wa Waisraeli aliyekufa. Lakini moyo wa Farao haukukubali kuwaachia watu waende.
8
Kisha Bwana akamwambia Mose na Aroni, “Chukueni majivu ya tanuru, naye Mose ayarushe angani mbele ya Farao.
9
Yatakuwa vumbi jepesi juu ya nchi yote ya Misri, pia yatatokea majipu yenye kufura juu ya watu na wanyama katika nchi yote.”
10
Basi wakachukua majivu kwenye tanuru na kusimama mbele ya Farao. Mose akayarusha hewani, nayo majipu yenye kufura yakatokea miilini mwa watu na wanyama.
11
Waganga hawakuweza kusimama mbele ya Mose kwa sababu ya majipu yale yaliyokuwa miilini mwao na juu ya miili ya Wamisri wote.
12
Lakini Bwana akaufanya moyo wa Farao kuwa mgumu, naye hakuwasikiliza Mose na Aroni, sawasawa kama vile Bwana alivyokuwa amemwambia Mose.
13
Kisha Bwana akamwambia Mose, “Amka mapema asubuhi, usimame mbele ya Farao, umwambie, ‘Hili ndilo asemalo Bwana, Mungu wa Waebrania: Waachie watu wangu waende, ili kwamba waweze kuniabudu,
14
au wakati huu nitaleta mapigo yangu yenye nguvu dhidi yako, maafisa wako na watu wako, ili upate kujua kuwa hakuna mwingine kama Mimi katika dunia yote.
15
Kwa kuwa mpaka sasa ningelikuwa nimenyoosha mkono wangu na kukupiga wewe na watu wako kwa pigo ambalo lingekufutilia mbali juu ya nchi.
Maandiko ya Biblia: Biblica® Open Kiswahili Contemporary Version (Neno: Bibilia Takatifu)™, © 1984, 1989, 2009, 2015 Biblica, Inc. · CC BY-SA 4.0“Biblica” is a trademark registered in the United States Patent and Trademark Office by Biblica, Inc., used with permission.
Settings