Kutoka 29:19-28
19
“Mchukue yule kondoo dume mwingine, naye Aroni na wanawe waweke mikono yao juu ya kichwa chake.
20
Mchinje, uchukue sehemu ya damu yake na kuipaka kwenye masikio ya Aroni na wanawe, kwenye vidole gumba vya mikono yao ya kuume, pia kwenye vidole gumba vya miguu yao ya kuume. Kisha nyunyiza hiyo damu pande zote za madhabahu.
21
Pia chukua sehemu ya damu iliyo juu ya madhabahu na sehemu ya mafuta ya upako, umnyunyizie Aroni na mavazi yake, pia wanawe na mavazi yao. Ndipo Aroni na wanawe pamoja na mavazi yao watakuwa wamewekwa wakfu.
22
“Chukua mafuta ya huyu kondoo dume, mafuta ya mkia, mafuta ya sehemu za ndani yale yanayofunika ini, figo zote mbili na mafuta yake, pamoja na paja la kulia. (Huyo ndiye kondoo dume kwa ajili ya kuwaweka wakfu.)
23
Kutoka kwenye kile kikapu chenye mikate iliyotengenezwa bila chachu, kilichoko mbele za Bwana, chukua mkate, andazi lililokandwa kwa mafuta na mkate mdogo mwembamba.
24
Viweke vitu hivi vyote mikononi mwa Aroni na wanawe na uviinue mbele za Bwana kuwa sadaka ya kuinuliwa.
25
Kisha vichukue vitu hivyo kutoka mikononi mwao, uviteketeze juu ya madhabahu pamoja na sadaka ya kuteketezwa kuwa harufu nzuri ya kupendeza kwa Bwana, sadaka iliyotolewa kwa Bwana kwa moto.
26
Baada ya kuchukua kidari cha huyo kondoo dume wa kuwekwa wakfu kwa Aroni, kiinue mbele za Bwana kuwa sadaka ya kuinuliwa, nayo itakuwa fungu lako.
27
“Weka wakfu zile sehemu za kondoo dume aliyetumika kwa kumweka wakfu Aroni na wanawe: kidari kile kilichoinuliwa na lile paja lililotolewa.
28
Siku zote hili litakuwa fungu la kawaida kutoka kwa Waisraeli kwa ajili ya Aroni na wanawe. Hili ni toleo la Waisraeli watakalotoa kwa Bwana kutoka sadaka zao za amani.
Settings