Kumbukumbu 21:1-9
1
Kama mtu akikutwa ameuawa, naye amelala kwenye shamba katika nchi ambayo Bwana Mungu wenu anawapa kuimiliki, wala haijulikani ni nani aliyemuua,
2
wazee wenu na waamuzi watatoka na kupima umbali kutoka maiti alipolala mpaka kwenye miji ya jirani.
3
Kisha wazee wa ule mji ulio karibu zaidi na yule maiti watamchukua mtamba ambaye hajapata kufanyishwa kazi na ambaye hajafungwa nira,
4
na kumpeleka kwenye bonde ambalo halijapata kulimwa au kupandwa mazao na ambapo kuna chemchemi itiririkayo. Huko kwenye hilo bonde, wazee watamvunja yule mtamba shingo.
5
Makuhani, hao wana wa Lawi, watasogea mbele, kwa kuwa Bwana Mungu wenu, amewachagua kuhudumu na kutoa baraka katika jina la Bwana, na kuamua mashauri yote ya mabishano na mashambulio.
6
Ndipo wazee wote wa mji ulio karibu zaidi na huyo maiti watanawa mikono yao juu ya huyo mtamba ambaye shingo yake imevunjwa huko kwenye bonde,
7
nao watatangaza: “Mikono yetu haikumwaga damu hii, wala macho yetu hayakuona likifanyika.
8
Ee Bwana, ukubali upatanisho kwa watu wako Israeli, ambao umewakomboa, wala usiwahesabie watu wako hatia ya damu ya mtu asiyekuwa na hatia.” Nayo damu iliyomwagika itakuwa imefanyiwa upatanisho.
9
Hivyo mtakuwa mmejitakasa wenyewe kutoka hatia ya kumwaga damu isiyokuwa na hatia, kwa kuwa mmefanya lile lililo sawa mbele za macho ya Bwana.
Settings