Skip to content
Kumbukumbu 12:5-18

Kumbukumbu 12:5-18

5
Bali mtatafuta mahali Bwana Mungu wenu atakapopachagua katika makabila yenu yote ili aliweke jina lake huko kuwa makao yake. Mahali hapo ndipo iwapasapo kwenda;
6
hapo ndipo mtakapoleta sadaka zenu za kuteketezwa na dhabihu, zaka zenu na changizo zenu, kile ulichoweka nadhiri kutoa, sadaka zenu za hiari na malimbuko ya makundi yenu ya ngʼombe pamoja na mbuzi na kondoo.
7
Hapo, katika uwepo wa Bwana Mungu wenu, ninyi pamoja na jamaa zenu, mtakula na kufurahia kila kitu ambacho mmegusa kwa mikono yenu, kwa sababu Bwana Mungu wenu amewabariki.
8
Msifanye kama tunavyofanya hapa leo, kila mtu anavyopenda mwenyewe,
9
kwa kuwa bado hamjafikia mahali pa mapumziko na urithi ambao Bwana Mungu wenu anawapa.
10
Lakini mtavuka Yordani na kuishi katika nchi Bwana Mungu wenu anayowapa kama urithi, naye atawapa pumziko kutokana na adui zenu wote wanaowazunguka ili ninyi mpate kuishi kwa salama.
11
Kisha kuhusu mahali Bwana Mungu wenu atakapopachagua kuwa mahali pa makao ya Jina lake, hapo ndipo inapowapasa kuleta kila kitu ninachowaamuru: sadaka zenu za kuteketezwa na dhabihu, zaka zenu na changizo, pamoja na vitu vyote vyenye thamani ambavyo mmeweka nadhiri kumtolea Bwana.
12
Hapo furahini mbele za Bwana Mungu wenu, ninyi, wana wenu na binti zenu, watumishi wenu wa kiume na wa kike, pamoja na Walawi kutoka miji yenu ambao hawana mgawo wala urithi wao wenyewe.
13
Kuweni waangalifu, msitoe dhabihu zenu za kuteketezwa mahali popote mnapopapenda.
14
Mtazitoa tu mahali pale ambapo Bwana atachagua katika mojawapo ya makabila yenu, nanyi hapo zingatieni kila jambo ninalowaamuru.
15
Hata hivyo, mnaweza kuwachinja wanyama wenu katika miji yenu yoyote ile na kula nyama nyingi mpendavyo kama vile mmemchinja paa au kulungu, kulingana na baraka mtakazojaliwa na Bwana Mungu wenu. Watu walio najisi au walio safi wanaweza kula.
16
Lakini kamwe usinywe damu; imwage juu ya ardhi kama maji.
17
Hamruhusiwi kula katika miji yenu zaka yenu ya nafaka, ya divai mpya na ya mafuta, au mzaliwa wa kwanza wa makundi yenu ya ngʼombe na makundi yenu ya mbuzi na kondoo, wala chochote ambacho mmeweka nadhiri kukitoa, au sadaka zako za hiari, wala matoleo maalum.
18
Badala yake, mtakula vitu hivyo katika uwepo wa Bwana Mungu wenu mahali ambapo Bwana Mungu wenu atapachagua: wewe, wana wako na binti zako, watumishi wako wa kiume na wa kike, na Walawi kutoka miji yenu. Mnatakiwa mfurahi mbele za Bwana Mungu wenu kwa kula kitu mtakachoweka mikono yenu.
Settings

Reading Style

Typeface

Font Size 19px

Options