Kumbukumbu 1:6-29
6
Bwana Mungu wetu alisema nasi huko Horebu, “Mmekaa vya kutosha katika mlima huu.
7
Vunjeni kambi, msonge mbele kuelekea nchi ya vilima ya Waamori; nendeni kwa watu wote ambao ni majirani wa Araba, katika milima, upande wa magharibi chini ya vilima, katika Negebu na kandokando ya pwani, mpaka nchi ya Wakanaani hadi Lebanoni, na kufika mto mkubwa Frati.
8
Tazama, nimewapa ninyi nchi hii. Ingieni mkaimiliki nchi ambayo Bwana aliapa kuwa angaliwapa baba zenu, Abrahamu, Isaki na Yakobo, pamoja na vizazi vyao baada yao.”
9
Wakati ule niliwaambia, “Ninyi mmekuwa mzigo mzito sana kwangu kuwachukua peke yangu.
10
Bwana Mungu wenu ameongeza hesabu yenu, hivi kwamba leo ninyi ni wengi kama nyota za angani.
11
Naye Bwana, Mungu wa baba zenu na awaongeze mara elfu na kuwabariki kama alivyoahidi!
12
Lakini mimi nitawezaje kubeba matatizo yenu, na mizigo yenu, na magomvi yenu peke yangu?
13
Chagueni baadhi ya watu wenye hekima, wenye ufahamu na wanaoheshimika kutoka kila kabila lenu, nami nitawaweka juu yenu.”
14
Mlinijibu, “Shauri ulilolitoa ni zuri.”
15
Kwa hiyo niliwachukua wanaume viongozi wa makabila yenu, wenye hekima na wanaoheshimika, nami nikawateua wawe na mamlaka juu yenu kama majemadari wa maelfu, wa mamia, wa hamsini, na wa makumi, na kama maafisa wa makabila.
16
Nami wakati ule nikawaagiza waamuzi wenu: Sikilizeni magomvi kati ya ndugu zenu na mwamue kwa haki, hata kama shauri ni kati ya ndugu wa Kiisraeli, au kati ya mmoja wa ndugu wa Kiisraeli na mgeni.
17
Msionyeshe upendeleo katika maamuzi; wasikilizeni wote sawasawa, wadogo kwa wakubwa. Msimwogope mtu yeyote, kwa kuwa hukumu ni ya Mungu. Mniletee mimi shauri lolote lililo gumu sana kwenu, nami nitalisikiliza.
18
Nami wakati ule niliwaambia kila kitu ambacho mngefanya.
19
Kisha, kama Bwana Mungu wetu alivyotuamuru, tuliondoka kutoka Horebu na kwenda kuelekea nchi ya vilima ya Waamori, kupitia jangwa lile kubwa lote la kutisha, lile mliloliona, nasi tukafika Kadesh-Barnea.
20
Kisha niliwaambia, “Mmefika katika nchi ya vilima ya Waamori, ambayo Bwana Mungu wetu anatupa.
21
Tazama, Bwana Mungu wenu amewapa nchi. Pandeni mkaimiliki kama Bwana, Mungu wa baba zenu, alivyowaambia. Msiogope, wala msikate tamaa.”
22
Ndipo ninyi nyote mkanijia na kusema, “Tupeleke watu watutangulie kuipeleleza nchi kwa ajili yetu, na kutuletea taarifa kuhusu njia tutakayopita, na miji tutakayoiendea.”
23
Wazo hilo lilionekana zuri kwangu; kwa hiyo niliwachagua watu wenu kumi na wawili, mwanaume mmoja kutoka kila kabila.
24
Waliondoka na kukwea katika nchi ya vilima, wakafika katika Bonde la Eshkoli na kuipeleleza.
25
Wakachukua baadhi ya matunda ya nchi, wakatuletea na kutuarifu, “Ni nchi nzuri ambayo Bwana Mungu wetu anatupa.”
26
Lakini hamkuwa tayari kukwea, mkaasi dhidi ya amri ya Bwana Mungu wenu.
27
Mkanungʼunika ndani ya mahema yenu na kusema, “Bwana anatuchukia, kwa hiyo alitutoa Misri ili kututia mikononi mwa Waamori kutuangamiza.
28
Twende wapi? Ndugu zetu wametufanya kufa moyo. Wanasema, ‘Watu wa huko wana nguvu zaidi na ni warefu kuliko sisi tulivyo; miji ni mikubwa, yenye kuta zilizofika juu angani. Zaidi ya hayo, tumewaona Waanaki huko.’ ”
29
Ndipo nikawaambia, “Msihofu, wala msiwaogope.
Settings