Skip to content
Danieli 7:1-14

Danieli 7:1-14

1
Katika mwaka wa kwanza wa utawala wa Belshaza mfalme wa Babeli, Danieli aliota ndoto, nayo maono yakapita mawazoni yake alipokuwa amelala kitandani mwake. Akayaandika mambo aliyoyaona katika ndoto yake.
2
Danieli akasema: “Katika maono yangu usiku nilitazama, na hapo mbele yangu kulikuwepo na upepo kutoka pande nne za mbingu, ukivuruga bahari kuu.
3
Wanyama wanne wakubwa, kila mmoja tofauti na mwenzake, wakajitokeza kutoka bahari.
4
“Mnyama wa kwanza alifanana na simba, naye alikuwa na mabawa kama ya tai. Nikatazama mpaka mabawa yake yalipongʼolewa, naye akainuliwa katika nchi, akasimama kwa miguu miwili kama mwanadamu, naye akapewa moyo wa binadamu.
5
“Hapo mbele yangu kulikuwa na mnyama wa pili, ambaye alionekana kama dubu. Upande wake mmoja ulikuwa umeinuka, na alikuwa na mbavu tatu katika kinywa chake kati ya meno yake. Akaambiwa, ‘Amka, ule nyama mpaka ushibe!’
6
“Baada ya huyo, nilitazama, na mbele yangu kulikuwa na mnyama mwingine, aliyefanana na chui. Juu ya mgongo wake alikuwa na mabawa manne kama ya ndege. Mnyama huyu alikuwa na vichwa vinne, naye akapewa mamlaka ya kutawala.
7
“Baada ya huyo, katika maono yangu usiku nilitazama, na mbele yangu kulikuwa na mnyama wa nne, mwenye kutisha na kuogofya, tena mwenye nguvu nyingi. Alikuwa na meno makubwa ya chuma; akapondaponda na kuangamiza wahanga wake, na kukanyaga chini ya nyayo zake chochote kilichosalia. Alikuwa tofauti na wanyama wote waliotangulia, naye alikuwa na pembe kumi.
8
“Wakati nilipokuwa ninafikiri kuhusu pembe hizo, mbele yangu kulikuwa na pembe nyingine, ambayo ni ndogo, iliyojitokeza miongoni mwa zile kumi; pembe tatu za mwanzoni zilingʼolewa ili kuipa nafasi hiyo ndogo. Pembe hii ilikuwa na macho kama ya mwanadamu, na mdomo ulionena kwa majivuno.
9
“Nilipoendelea kutazama, “viti vya enzi vikawekwa, naye Mzee wa Siku akaketi. Mavazi yake yalikuwa meupe kama theluji; nywele za kichwa chake zilikuwa nyeupe kama sufu. Kiti chake cha enzi kilikuwa kinawaka kwa miali ya moto, nayo magurudumu yake yote yalikuwa yanawaka moto.
10
Mto wa moto ulikuwa unatiririka, ukipita mbele yake. Maelfu elfu wakamhudumia; kumi elfu mara kumi elfu wakasimama mbele zake. Mahakama ikakaa kuhukumu, na vitabu vikafunguliwa.
11
“Kisha nikaendelea kutazama kwa sababu ya yale maneno ya majivuno yaliyosemwa na ile pembe. Nikaendelea kuangalia mpaka yule mnyama alipouawa, na mwili wake ukaharibiwa na kutupwa katika ule moto uliowaka.
12
(Wanyama wengine walikuwa wamevuliwa mamlaka yao, lakini waliruhusiwa kuishi kwa muda fulani.)
13
“Katika maono yangu ya usiku nilitazama, na mbele yangu nikamwona anayefanana na mwanadamu, akija pamoja na mawingu ya mbinguni. Akamkaribia huyo Mzee wa Siku, na akaongozwa mbele zake.
14
Akapewa mamlaka, utukufu na ufalme wenye nguvu; nao watu wa kabila zote, mataifa, na watu wa kila lugha wakamwabudu. Utawala wake ni utawala wa milele ambao hautapita, nao ufalme wake ni ule ambao kamwe hautaangamizwa.
Settings

Reading Style

Typeface

Font Size 19px

Options