2 Samweli 16:1-4
1
Daudi alipokuwa amekwenda umbali mfupi kupita kilele cha mlima, akamkuta huko Siba, msimamizi wa shughuli za Mefiboshethi, akingojea kumlaki Daudi. Alikuwa na punda wawili wakiwa wametandikwa na kupakiwa mikate mia mbili, maandazi mia ya zabibu kavu, maandazi mia ya tini na kiriba cha divai.
2
Mfalme Daudi akamuuliza Siba, “Kwa nini umeleta vitu hivi?” Siba akamjibu, “Punda ni kwa ajili ya watu wa nyumba ya mfalme kupanda, mikate na matunda ni kwa ajili ya watu kula, nayo divai ni kwa kuwaburudisha watakaochoka jangwani.”
3
Kisha mfalme akauliza, “Yuko wapi mwana wa bwana wako?” Siba akamwambia, “Anakawia Yerusalemu, kwa sababu anafikiri, ‘Leo nyumba ya Israeli itanirudishia utawala wa baba yangu.’ ”
4
Ndipo mfalme akamwambia Siba, “Yote yaliyokuwa mali ya Mefiboshethi sasa ni mali yako.” Siba akasema, “Nasujudu kwa unyenyekevu. Naomba nipate kibali mbele yako, bwana wangu mfalme.”
Settings