2 Samweli 14:11-20
11
Huyo mwanamke akasema, “Basi mfalme na amwombe Bwana Mungu wake ili kuzuia mlipiza kisasi cha damu kuongeza juu ya uharibifu, ili kwamba mwanangu asije akaangamizwa.” Mfalme akasema, “Hakika kama aishivyo Bwana, hakuna unywele mmoja wa kichwa cha mwanao utakaoanguka chini.”
12
Ndipo huyo mwanamke akasema, “Mruhusu mtumishi wako aseme neno kwa mfalme bwana wangu.” Mfalme akajibu, “Sema.”
13
Huyo mwanamke akasema, “Mbona basi wewe umewaza jambo kama hili dhidi ya watu wa Mungu? Je, mfalme asemapo hili, hajitii hatiani mwenyewe, kwa maana mfalme hajamrudisha mwanawe aliyefukuziwa mbali?
14
Kama vile maji yaliyomwagika ardhini, yasivyoweza kuzoleka tena, hivyo sisi kufa ni lazima. Lakini Mungu haondoi uhai, badala yake, yeye hufanya njia ili kwamba aliyefukuzwa asibaki akiwa amefarikishwa naye.
15
“Nami sasa nimekuja kusema hili kwa bwana wangu mfalme kwa sababu watu wameniogopesha. Mtumishi wako alifikiri, ‘Nitanena na mfalme, labda mfalme atamfanyia mtumishi wake kile anachoomba.
16
Labda mfalme atakubali kumwokoa mtumishi wake kutoka mkononi mwa mtu anayejaribu kunikatilia mbali, mimi na mwanangu, kutoka kwenye urithi Mungu aliotupatia.’
17
“Basi sasa mtumishi wako anasema, ‘Neno la bwana wangu mfalme na linipatie pumziko, kwa maana bwana wangu mfalme ni kama malaika wa Mungu katika kutambua jema na baya. Bwana Mungu wako na awe pamoja nawe.’ ”
18
Basi mfalme akamwambia huyo mwanamke, “Usinifiche jibu kuhusu hilo nitakalokuuliza.” Huyo mwanamke akasema, “Mfalme bwana wangu na aseme.”
19
Mfalme akauliza, “Je, mkono wa Yoabu haupo pamoja nawe katika jambo hilo lote?” Huyo mwanamke akajibu, “Hakika kama uishivyo, bwana wangu mfalme, hakuna yeyote anayeweza kugeuka kulia wala kushoto kutokana na chochote anachosema bwana wangu mfalme. Naam, ni mtumishi wako Yoabu ndiye alinifundisha kufanya hivi, naye ndiye aliweka maneno haya yote kinywani mwa mtumishi wako.
20
Mtumishi wako Yoabu amefanya hivi ili kubadili hali iliyopo. Bwana wangu ana hekima kama ile ya malaika wa Mungu, hufahamu kila kitu kinachotokea katika nchi.”
Settings