Skip to content
2 Wafalme 6:24-33

2 Wafalme 6:24-33

24
Baada ya kitambo kidogo, Ben-Hadadi mfalme wa Aramu akaandaa jeshi lake lote akapanda kwenda kuihusuru Samaria.
25
Kukawa na njaa kuu katika mji. Samaria ilizingirwa kwa muda mrefu, kiasi kwamba kichwa cha punda kiliuzwa kwa shekeli themanini za fedha, na robo ya kibaba cha mavi ya njiwa kiliuzwa kwa shekeli tano za fedha.
26
Wakati mfalme wa Israeli alipokuwa anapita juu ya ukuta, mwanamke mmoja akamlilia, “Bwana wangu mfalme, nisaidie!”
27
Mfalme akajibu, “Ikiwa Bwana hakusaidii, nitakutolea wapi msaada? Je, ni kutoka kwenye sakafu ya kupuria? Au kwenye shinikizo la divai?”
28
Kisha akamuuliza, “Kwani kuna nini?” Yule mwanamke akamjibu, “Huyu mwanamke aliniambia, ‘Mtoe mwanao ili tupate kumla leo, na kesho tutamla mwanangu.’
29
Basi tukampika mwanangu na kumla. Siku iliyofuata nikamwambia, ‘Mtoe mwanao ili tupate kumla.’ Lakini akawa amemficha.”
30
Wakati mfalme aliposikia maneno ya yule mwanamke, alirarua mavazi yake. Naye alipoendelea kutembea ukutani, watu wakamtazama, na ndani ya mavazi yake alikuwa amevaa nguo ya gunia mwilini mwake.
31
Akasema, “Mungu na anitendee hivyo na kuzidi, ikiwa kichwa cha Elisha mwana wa Shafati kitabaki juu ya mabega yake leo!”
32
Wakati huu, Elisha alikuwa ameketi ndani ya nyumba yake, akiwa pamoja na wazee. Mfalme akatuma mjumbe kumtangulia, lakini kabla hajafika, Elisha akawaambia wale wazee, “Hammwoni huyu muuaji jinsi anavyotuma mtu kukata kichwa changu? Tazama, wakati mjumbe huyo atakapofika, fungeni mlango na mzuieni asiingie. Je, vishindo vya nyayo za bwana wake haviko nyuma yake?”
33
Alipokuwa angali bado anazungumza nao, mjumbe akamfikia. Naye mfalme akasema, “Maafa haya yanatoka kwa Bwana. Kwa nini niendelee kumngoja Bwana zaidi?”
Settings

Reading Style

Typeface

Font Size 19px

Options