2 Wafalme 18:17-26
17
Mfalme wa Ashuru akamtuma jemadari wake mkuu, na afisa wake mkuu, na jemadari wa jeshi, pamoja na jeshi kubwa kutoka Lakishi hadi kwa Mfalme Hezekia huko Yerusalemu. Wakaja Yerusalemu na kusimama kwenye mfereji wa Bwawa la Juu, lililojengwa katika barabara iendayo kwenye Uwanja wa Dobi.
18
Wakaagiza mfalme aitwe. Eliakimu mwana wa Hilkia aliyekuwa msimamizi wa jumba la mfalme, Shebna aliyekuwa katibu, na Yoa mwana wa Asafu mwandishi wakawaendea.
19
Yule jemadari wa jeshi akawaambia, “Mwambieni Hezekia: “ ‘Hili ndilo asemalo mfalme mkuu, mfalme wa Ashuru: Ni wapi unapoweka hili tumaini lako?
20
Unasema mnayo mikakati na nguvu za kijeshi, lakini unasema maneno matupu tu. Je, wewe unamtegemea nani, hata ukaniasi mimi?
21
Tazama sasa, unaitegemea Misri, fimbo ile ya mwanzi uliopasuka, ambayo huuchoma na kuujeruhi mkono wa mtu akiiegemea! Hivyo ndivyo alivyo Farao mfalme wa Misri, kwa wote wanaomtegemea.
22
Nawe kama ukiniambia, “Tunamtumainia Bwana Mungu wetu”: je, siyo yeye ambaye Hezekia aliondoa mahali pake pa juu pa kuabudia miungu na madhabahu zake, akiwaambia Yuda na Yerusalemu, “Ni lazima mwabudu mbele ya madhabahu haya katika Yerusalemu”?
23
“ ‘Njooni sasa, fanyeni mapatano na bwana wangu, mfalme wa Ashuru: Nitakupa farasi elfu mbili, kama unaweza kuwapandisha waendesha farasi juu yao!
24
Utawezaje kumzuia hata afisa mmoja aliye mdogo kati ya maafisa wa bwana wangu, ijapo unategemea Misri kwa magari ya vita na wapanda farasi?
25
Zaidi ya hayo, je, nimekuja kushambulia na kuangamiza mahali hapa pasipo neno kutoka kwa Bwana? Bwana mwenyewe ndiye aliniambia niishambulie nchi hii na kuiangamiza.’ ”
26
Ndipo Eliakimu mwana wa Hilkia, Shebna na Yoa wakamwambia yule jemadari wa jeshi, “Tafadhali zungumza na watumishi wako kwa lugha ya Kiaramu, kwa kuwa tunaifahamu. Usiseme nasi kwa Kiebrania watu walioko juu ya ukuta wakiwa wanasikia.”
Settings