Nehemia 9:15-25
15
Katika njaa yao uliwapa mkate kutoka mbinguni, na katika kiu yao uliwatolea maji kutoka kwenye mwamba. Uliwaambia waingie na kuimiliki nchi ambayo ulikuwa umeapa kuwapa kwa mkono ulioinuliwa.
16
“Lakini wao, baba zetu, wakawa na kiburi na shingo ngumu, nao hawakutii maagizo yako.
17
Wakakataa kusikiliza na kushindwa kukumbuka miujiza uliyoifanya miongoni mwao. Wakawa na shingo ngumu, na katika uasi wao wakamchagua kiongozi ili warudi kwenye utumwa wao. Lakini wewe ni Mungu mwenye kusamehe, mwenye neema na mwingi wa huruma, si mwepesi wa hasira, ni mwingi wa upendo. Kwa hiyo hukuwaacha,
18
hata wakati walijitengenezea sanamu ya ndama ya kusubu na kusema, ‘Huyu ni mungu wenu, aliyewapandisha kutoka nchi ya Misri,’ au walipofanya makufuru makubwa.
19
“Kwa sababu ya huruma zako kuu hukuwaacha jangwani. Wakati wa mchana ile nguzo ya wingu haikukoma kuwaongoza katika njia yao, wala nguzo ya moto haikuacha kuwamulikia usiku njia iliyowapasa kuiendea.
20
Uliwapa Roho wako mwema ili kuwafundisha. Hukuwanyima mana yako vinywani mwao, nawe ukawapa maji kwa ajili ya kiu yao.
21
Kwa miaka arobaini uliwatunza jangwani. Hawakukosa chochote, na nguo zao hazikuchakaa wala miguu yao haikuvimba.
22
“Uliwapa falme na mataifa, ukiwagawia hata mipaka ya mbali. Wakaimiliki nchi ya Sihoni mfalme wa Heshboni, na nchi ya Ogu mfalme wa Bashani.
23
Uliwafanya wana wao kuwa wengi kama nyota za angani, nawe ukawaleta katika nchi ambayo uliwaambia baba zao kuingia na kuimiliki.
24
Wana wao wakaingia na kuimiliki nchi. Uliwatiisha Wakanaani mbele yao, walioishi katika nchi, ukawatia Wakanaani mikononi mwao, pamoja na wafalme wao na watu wa nchi, wawafanyie kama wapendavyo.
25
Wakateka miji yenye ngome na nchi yenye rutuba, wakamiliki nyumba zilizojazwa na vitu vizuri vya kila aina, visima vilivyochimbwa tayari, mashamba ya mizabibu, mashamba ya mizeituni na miti yenye matunda kwa wingi. Wakala, wakashiba nao wakanawiri sana, wakajifurahisha katika wema wako mwingi.
Settings