Nehemia 13:15-22
15
Siku hizo nikaona watu katika Yuda wakikanyaga mashinikizo ya divai siku ya Sabato na kuleta nafaka wakiwapakiza punda, pamoja na divai, zabibu, tini na aina nyingine za mizigo. Nao walikuwa wakileta haya yote Yerusalemu siku ya Sabato. Kwa hiyo niliwaonya dhidi ya kuuza vyakula siku hiyo.
16
Watu kutoka Tiro waliokuwa wakiishi Yerusalemu walileta samaki na aina nyingi za bidhaa na kuziuza Yerusalemu siku ya Sabato kwa watu wa Yuda.
17
Niliwakemea wakuu wa Yuda na kuwaambia, “Ni uovu gani huu mnaofanya wa kuinajisi siku ya Sabato?
18
Je, baba zenu hawakufanya mambo kama haya, hata wakamsababisha Mungu wetu kuleta maafa haya yote juu yetu na juu ya mji huu? Sasa bado mnazidi kuchochea ghadhabu yake dhidi ya Israeli kwa kuinajisi Sabato.”
19
Wakati vivuli vya jioni vilipoangukia juu ya malango ya Yerusalemu kabla ya Sabato, niliamuru milango ifungwe, wala isifunguliwe mpaka Sabato iishe. Nikawaweka baadhi ya watu wangu mwenyewe kwenye malango ili pasiwepo mzigo utakaoingizwa ndani siku ya Sabato.
20
Mara moja au mbili wachuuzi na wauzaji wa bidhaa za aina zote walilala usiku nje ya mji wa Yerusalemu.
21
Lakini niliwaonya na kuwaambia, “Kwa nini mnalala karibu na ukuta? Kama mkifanya hivi tena, nitawaadhibu.” Kuanzia wakati ule hawakuja tena siku ya Sabato.
22
Kisha nikawaamuru Walawi kujitakasa na kwenda kulinda malango ili kutunza Sabato iwe takatifu. Ee Mungu wangu, unikumbuke kwa ajili ya hili pia, nawe unionyeshe wema wako sawasawa na upendo wako mkuu.
Settings