Nehemia 10:32-39
32
“Tunakubali wajibu wa kutimiza amri za kutoa theluthi ya shekeli kila mwaka kwa ajili ya utumishi wa nyumba ya Mungu:
33
Kwa ajili ya mikate ya Wonyesho, kwa ajili ya sadaka za kawaida za nafaka na sadaka za kuteketezwa, kwa ajili ya sadaka za siku za Sabato, Sikukuu za Mwandamo wa Mwezi na sikukuu nyingine zilizoamriwa, kwa ajili ya sadaka takatifu, kwa ajili ya sadaka za dhambi ili kufanya upatanisho kwa ajili ya Israeli, na kwa ajili ya kazi zote za nyumba ya Mungu wetu.
34
“Sisi makuhani, Walawi na watu, tumepiga kura kuamua kuwa kila mmoja wa jamaa zetu lazima alete katika nyumba ya Mungu wetu kwa nyakati maalum kila mwaka mchango wa kuni za kukokea moto katika madhabahu ya Bwana Mungu wetu, kama ilivyoandikwa katika Sheria.
35
“Pia tunachukua wajibu wa kuleta malimbuko ya mazao yetu na matunda ya kwanza ya kila mti wa matunda katika nyumba ya Bwana kila mwaka.
36
“Kama pia ilivyoandikwa katika Sheria, tutawaleta wazaliwa wetu wa kwanza wa kiume, na wa mifugo yetu, yaani wa ngʼombe wetu na wa makundi yetu ya kondoo na mbuzi, katika nyumba ya Mungu wetu, kwa ajili ya makuhani wanaohudumu huko.
37
“Zaidi ya hayo, tutaleta katika ghala za nyumba ya Mungu wetu, kwa makuhani, vyakula vya kwanza vya mashamba yetu, sadaka zetu za nafaka, matunda ya miti yetu yote, divai yetu mpya na mafuta. Nasi tutaleta zaka za mazao yetu kwa Walawi, kwa kuwa Walawi ndio ambao hukusanya zaka katika miji yote tunakofanya kazi.
38
Kuhani atokanaye na uzao wa Aroni atashirikiana na Walawi wakati wanapopokea zaka, nao Walawi itawapasa kuleta sehemu ya kumi ya zaka katika nyumba ya Mungu wetu katika ghala za hazina.
39
Watu wa Israeli pamoja na Walawi itawapasa kuleta michango yao ya nafaka, divai mpya na mafuta katika vyumba vya ghala, mahali vifaa vya mahali patakatifu vinapohifadhiwa, na wanapokaa makuhani wanaohudumu, na mabawabu na waimbaji. “Hatutaacha kuijali nyumba ya Mungu wetu.”
Settings