Walawi 16:1-19
1
Bwana akasema na Mose baada ya kifo cha wale wana wawili wa Aroni waliokufa walipokaribia mbele za Bwana.
2
Bwana akamwambia Mose: “Mwambie ndugu yako Aroni asije wakati wowote atakavyo yeye ndani ya Patakatifu pa Patakatifu, nyuma ya pazia pale mbele ya kiti cha rehema kile kilichoko juu ya Sanduku la Agano, la sivyo atakufa, kwa sababu huwa ninatokea ndani ya wingu juu ya kile kiti cha rehema.
3
“Hivi ndivyo Aroni atakavyoingia katika mahali patakatifu: atachukua fahali mchanga kwa ajili ya sadaka ya dhambi, na kondoo dume kwa ajili ya sadaka ya kuteketezwa.
4
Atavaa koti takatifu la kitani, pamoja na nguo za ndani za kitani; atafunga mshipi wa kitani kiunoni, na kuvaa kilemba cha kitani. Haya ni mavazi matakatifu, kwa hiyo ni lazima aoge kwa maji kabla ya kuyavaa mavazi hayo.
5
Atachukua mbuzi dume wawili kutoka kwa jumuiya ya Israeli kwa ajili ya sadaka ya dhambi, na kondoo dume kwa ajili ya sadaka ya kuteketezwa.
6
“Aroni atamtoa huyo fahali kwa ajili ya sadaka yake ya dhambi ili afanye upatanisho kwa ajili yake mwenyewe na nyumba yake.
7
Kisha atawachukua wale mbuzi dume wawili na kuwaleta mbele za Bwana kwenye ingilio la Hema la Kukutania.
8
Aroni atapiga kura kwa ajili ya hao mbuzi wawili, mmoja kwa ajili ya Bwana na mwingine kwa ajili ya kubebeshwa dhambi.
9
Aroni atamleta yule mbuzi ambaye kura ya Bwana imemwangukia na kumtoa dhabihu kwa ajili ya sadaka ya dhambi.
10
Lakini mbuzi aliyechaguliwa kwa kura kuwa wa kubebeshwa dhambi atatolewa akiwa hai mbele za Bwana, atumike kwa kufanya upatanisho kwa kumwacha aende jangwani akiwa amebebeshwa dhambi.
11
“Aroni atamleta yule fahali kwa ajili ya sadaka ya dhambi yake mwenyewe, ili kufanya upatanisho kwa ajili yake na nyumba yake, naye atamchinja huyo fahali kwa ajili ya sadaka ya dhambi yake mwenyewe.
12
Atachukua chetezo kilichojaa makaa yanayowaka kutoka madhabahuni mbele za Bwana, na konzi mbili za uvumba laini uliosagwa vizuri wenye harufu, na kuvipeleka nyuma ya pazia.
13
Ataweka uvumba juu ya moto mbele za Bwana, na moshi wa uvumba utafunika kile kiti cha rehema kilicho juu ya Ushuhuda, ili asife.
14
Atachukua sehemu ya damu ya fahali, na kwa kidole chake atanyunyiza sehemu ya mbele ya kiti cha rehema; kisha atanyunyiza sehemu ya hiyo damu kwa kidole chake mara saba mbele ya kiti cha rehema.
15
“Kisha atamchinja mbuzi wa sadaka ya dhambi kwa ajili ya watu, na kuichukua damu yake nyuma ya pazia, na aifanyie kama alivyofanya kwa damu ya fahali: Atanyunyiza juu ya kiti cha rehema na mbele yake.
16
Kwa njia hii atafanya upatanisho kwa ajili ya Patakatifu pa Patakatifu kwa sababu ya unajisi na uasi wa Waisraeli, kwa dhambi zao zozote. Atafanya hivyo kwa ajili ya Hema la Kukutania, ambalo liko miongoni mwao katikati ya unajisi wao.
17
Mtu yeyote haruhusiwi kuwa ndani ya Hema la Kukutania, kuanzia wakati Aroni anapoingia kufanya upatanisho katika Patakatifu pa Patakatifu, hadi atakapotoka nje, baada ya kujifanyia upatanisho yeye mwenyewe na nyumba yake, pamoja na jumuiya yote ya Israeli.
18
“Kisha atatoka aje kwenye madhabahu yaliyo mbele za Bwana na kufanya upatanisho kwa ajili yake. Atachukua sehemu ya damu ya fahali na sehemu ya damu ya mbuzi, na kuiweka kwenye pembe za madhabahu.
19
Atanyunyiza baadhi ya hiyo damu juu ya madhabahu kwa kidole chake mara saba, ili kuitakasa na kuiweka wakfu kutokana na unajisi wa Waisraeli.
Settings