Skip to content
Walawi 15:20-33

Walawi 15:20-33

20
“ ‘Chochote atakacholalia wakati wake wa hedhi kitakuwa najisi, na chochote atakachokikalia kitakuwa najisi.
21
Yeyote atakayegusa kitanda chake ni lazima afue nguo zake na aoge kwa maji, naye atakuwa najisi mpaka jioni.
22
Yeyote atakayegusa chochote atakachokalia ni lazima afue nguo zake na aoge kwa maji, naye atakuwa najisi mpaka jioni.
23
Kiwe ni kitanda ama chochote alichokuwa amekikalia, ikiwa mtu yeyote atakigusa, atakuwa najisi mpaka jioni.
24
“ ‘Ikiwa mwanaume atalala naye na ile damu ya mwezi ikamgusa, atakuwa najisi kwa siku saba; kitanda chochote atakachokilalia huyo mwanaume kitakuwa najisi.
25
“ ‘Ikiwa mwanamke atatokwa na damu kwa siku nyingi zaidi ya siku zake za mwezi, au amekuwa na damu inayoendelea zaidi ya kipindi chake, atakuwa najisi kwa kipindi chote cha shida hiyo, kama ilivyokuwa katika siku za hedhi yake.
26
Kitanda chochote atakachokilalia huyo mwanamke wakati anaendelea kutokwa na damu kitakuwa najisi, kama kilivyokuwa kitanda chake wakati wa siku zake za hedhi, na chochote atakachokalia kitakuwa najisi, kama wakati wake wa hedhi.
27
Yeyote agusaye vitu hivyo atakuwa najisi; ni lazima afue nguo zake na kuoga kwa maji, naye atakuwa najisi mpaka jioni.
28
“ ‘Wakati atakapotakasika kutoka hedhi yake, ni lazima ahesabu siku saba, na baada ya hapo atakuwa safi kwa kawaida ya ibada.
29
Siku ya nane ni lazima achukue hua wawili au makinda mawili ya njiwa, na kumletea kuhani kwenye mlango wa Hema la Kukutania.
30
Kuhani atatoa dhabihu, mmoja kwa ajili ya sadaka ya dhambi, na huyo mwingine kwa ajili ya sadaka ya kuteketezwa. Kwa njia hii, atafanya upatanisho kwa ajili yake mbele za Bwana kwa sababu ya unajisi wa kutokwa damu kwake.
31
“ ‘Ni lazima uwatenge Waisraeli kutokana na vitu ambavyo vinawafanya najisi, ili wasife katika unajisi wao kwa kunajisi makao yangu, ambayo yapo katikati yao.’ ”
32
Haya ni masharti kwa ajili ya mtu mwenye kutokwa na usaha, kwa ajili ya yeyote atakayetokwa na shahawa,
33
kwa ajili ya mwanamke katika siku zake za hedhi, kwa ajili ya mwanaume au mwanamke atokwaye na usaha, na kwa ajili ya mwanaume alalaye na mwanamke ambaye ni najisi kwa kawaida ya ibada.
Settings

Reading Style

Typeface

Font Size 19px

Options