Walawi 14:1-20
1
Bwana akamwambia Mose,
2
“Haya ndiyo masharti yamhusuyo mtu mgonjwa wakati wa kufanyiwa ibada ya utakaso wakati aletwapo kwa kuhani:
3
Kuhani atakwenda kumchunguza nje ya kambi. Kama mtu huyo atakuwa amepona ugonjwa wake wa ngozi wa kuambukiza,
4
kuhani ataagiza vitu vifuatavyo viletwe kwa ajili ya mtu atakayetakaswa: ndege wawili safi walio hai, mti wa mwerezi, kitani nyekundu, na hisopo.
5
Kisha kuhani ataagiza kwamba mmoja wa ndege wale achinjwe kwenye chungu chenye maji safi.
6
Kisha kuhani atamchukua ndege aliye hai na kumtumbukiza pamoja na mti wa mwerezi, kitani nyekundu na hisopo ndani ya damu ya yule ndege aliyechinjiwa kwenye maji safi.
7
Atamnyunyizia yule mwenye ugonjwa wa kuambukiza maji hayo mara saba, na kumtangaza kuwa safi. Kisha atamwachia yule ndege aliye hai aende zake kwenye mashamba.
8
“Huyo mtu atakayetakaswa ni lazima afue nguo zake, anyoe nywele zake zote, na aoge kwa maji; ndipo atakapokuwa safi kwa desturi ya ibada. Baada ya hili anaweza kuingia kambini, lakini ni lazima akae nje ya hema lake kwa siku saba.
9
Siku ya saba ni lazima anyoe nywele zake zote; yaani anyoe nywele za kichwa, ndevu zake, kope zake na nywele nyingine zote. Ni lazima afue nguo zake, na aoge kwa maji, naye atakuwa safi.
10
“Siku ya nane, ni lazima alete kondoo dume wawili na kondoo jike mmoja, wote wa mwaka mmoja na wasio na dosari, pamoja na sehemu tatu za kumi za efa za unga laini uliochanganywa na mafuta, kwa ajili ya sadaka ya nafaka, na logi moja ya mafuta.
11
Kuhani atakayemtangaza kuwa safi atahitaji kumkabidhi mgonjwa aliyepona pamoja na sadaka zake zote mbele za Bwana katika ingilio la Hema la Kukutania.
12
“Kisha kuhani atamchukua mmoja wa wale kondoo dume na kumtoa kuwa sadaka ya hatia, pamoja na ile logi moja ya mafuta; ataviinua mbele za Bwana kuwa sadaka ya kuinuliwa.
13
Atamchinja huyo kondoo katika mahali patakatifu ambapo sadaka ya dhambi na ile ya kuteketezwa huchinjiwa. Kama ilivyo sadaka ya dhambi, sadaka ya hatia ni ya kuhani; nayo ni takatifu sana.
14
Kuhani atachukua sehemu ya damu ya sadaka ya hatia na kuitia kwenye ncha ya sikio la kuume la yule atakayetakaswa, kwenye kidole gumba cha mkono wake wa kuume, na kidole kikubwa cha mguu wake wa kuume.
15
Kuhani atachukua sehemu ya ile logi ya mafuta, ayamimine kwenye kiganja cha mkono wake mwenyewe wa kushoto,
16
na achovye kidole chake cha shahada cha mkono wake wa kuume kwenye mafuta yaliyoko kwenye kiganja chake, na kwa kidole hicho anyunyize mafuta hayo mara saba mbele za Bwana.
17
Kuhani atampaka yule anayetakaswa sehemu ya mafuta yaliyobaki kiganjani kwenye ncha ya sikio lake la kuume, kwenye kidole gumba cha mkono wake wa kuume, na kidole kikubwa cha mguu wake wa kuume, mahali palepale alipompaka damu ya sadaka ya kuondoa hatia.
18
Kuhani atayapaka mafuta yaliyobaki kwenye kiganja chake juu ya kichwa cha yule anayetakaswa, na kufanya upatanisho kwa ajili yake mbele za Bwana.
19
“Kisha kuhani atatoa dhabihu ya sadaka ya dhambi na kufanya upatanisho kwa ajili ya yule atakayetakaswa kutoka unajisi wake. Baada ya hayo, kuhani atachinja sadaka ya kuteketezwa
20
na kuitoa juu ya madhabahu, pamoja na sadaka ya nafaka ili kumfanyia upatanisho, naye atakuwa safi.
Settings