Walawi 10:12-20
12
Mose akamwambia Aroni pamoja na wanawe waliosalia, Eleazari na Ithamari, “Chukueni sadaka ya nafaka iliyobaki kutoka sadaka zilizotolewa kwa Bwana kwa moto, muile hapo kando ya madhabahu ikiwa imeandaliwa bila chachu, kwa sababu ni takatifu sana.
13
Mtaila katika mahali patakatifu kwa sababu ni fungu lenu na fungu la wana wenu la sadaka zilizotolewa kwa Bwana kwa moto, kwa maana hivyo ndivyo nilivyoamriwa.
14
Lakini wewe na wanao na binti zako mwaweza kula kidari kile kilichoinuliwa na paja lile lililotolewa. Mtavila mahali safi pa kawaida ya ibada; mmepewa wewe na watoto wako kuwa fungu lenu la sadaka za amani za Waisraeli.
15
Paja lile lililotolewa na kidari kile kilichoinuliwa lazima viletwe pamoja na sehemu za mafuta ya sadaka za kuteketezwa kwa moto, ili kuinuliwa mbele za Bwana kama sadaka ya kuinuliwa. Hili litakuwa fungu lako la kawaida na wanao, kama Bwana alivyoagiza.”
16
Mose alipouliza kuhusu mbuzi atolewaye kwa ajili ya sadaka ya dhambi, na kukuta kwamba ameteketezwa, aliwakasirikia Eleazari na Ithamari, wana wa Aroni waliobaki, akawauliza,
17
“Kwa nini hamkula sadaka ya dhambi katika eneo la mahali patakatifu? Ni takatifu sana. Mlipewa ninyi ili kuondoa hatia ya jumuiya kwa ajili ya kuwafanyia upatanisho mbele za Bwana.
18
Kwa kuwa damu yake haikuletwa ndani ya Mahali Patakatifu, mngemla mbuzi huyo katika sehemu ya mahali patakatifu kama nilivyoagiza.”
19
Aroni akamjibu Mose, “Leo wanangu wametoa sadaka zao za dhambi na sadaka zao za kuteketezwa mbele za Bwana, lakini mambo kama haya yamenitokea mimi. Je, Bwana angependezwa kama ningekuwa nimekula sadaka ya dhambi leo?”
20
Mose aliposikia haya, akaridhika.
Settings